Sunday, October 12, 2014

BENKI YA KIARABU YA MAENDELEO YA UCHUMI YA AFRIKA (BADEA) YATOA DOLA ZA KIMAREKANI MILIONI 12.0 SAWA NA FEDHA ZA KITANZANIA SHILINGI BILIONI 20.1 KUSAIDIA MAENDELEO KATIKA WILAYA YA SAMA NA MWANGA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr. Servacius Likwelile  na Eng. Yousef I. Al-Bassam ambaye ni Makamu wa Mwenyekiti  na Mkurugenzi Msimamizi wa mfuko wa maendeleo wa Saudia, wakibadilishana mikataba hiyo baada ya kutiliana saini.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa serikali  Dr. Servacius Likwelile, mchana wa leo ametiliana saini makubaliano ya mkataba wa kuanzisha Mradi wa Maji katika Wilaya ya Same na Mwanga. Dr. Likwelile alisaini Mkataba huo kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Kiarabu ya Maendeleo ya uchumi ya Afrika . 
Aliye wakilisha Benki hiyo ni Eng. Yousef I. Al-Bassam ambaye ni Makamu wa Mwenyekiti  na Mkurugenzi Msimamizi wa mfuko wa maendeleo wa Saudia.  
Aidha katika kutiliana saini Mkataba huo Dr. Likwelile alimueleza Eng. Yousef I. Al-Bassam  kuwa Serikali ya Tanzania inatambua kuwa BADEA  imetoa Dola za Kimarekani milioni 12.0 sawa na shilingi Bilioni 20.1 za Kitanzania kwa ajili ya kusaidia mradi wa maji katika Wilaya ya Same na Mwanga. Hivyo inatoa shukrani zake za dhati kwa BADEA kwa kusaidia kuchochea maendeleo ya Tanzania. 
“Msaada huu tulioupata leo utaisaidia Serikali kutatua tatizo la maji katika wilaya ya Same na Mwanga, hii inaonyesha  ni jinsi BADEA unaunga mkono na kutekeleza jukumu zima la kushiriki katika masuala ya kijamii na ya kiuchumi kwa nchi yetu ya Tanzania, hivyo tunaomba muendelee kutusaidia”. Alisema Dr. Likwelile. 
Dr. Likwelile alimueleza  Eng. Yousef I. Al-Bassam  kuwa, kama anavyofahamu  gharama za mapendekezo ya mradi mzima ni Dola za Kimarekani  million 110.43 na hii inahitaji uchangiaji kutoka katika mifuko mingine kama mfuko wa maendeleo wa Saudia , Mfuko wa Kimataifa wa OPEC  na Serikali kuchangia fedha kusaidia mradi huu. Kwa hili sina wasiwasi nalo kwani ninafuraha kujua kwamba umeshakubaliana na ninaujasiri kuwa jitihada zako zitafanikiwa.
“Mradi huu wa  maji wq wilaya ya Same na Mwanga unalenga kusaidia kuwepo kwa maji kwenye jamii mbalimbali zilizopo kwenye mradi huo.” Aliongeza Dr.Likwelile.
Aliendelea kusema kuwa,mradi huo utakapo kamilika :
(i) utaongeza kiwango cha watu wengi kuweza kupata maji safi na salama ya  kunywa.
(ii) Uchumi wa Same na Mwanga utaimarika pamoja na hali ya afya kwa jamii nayo itakuwa imara hasa kwa maeneo yale yanayoguswa na mradi.
(iii) Hali ya maisha ya watu wa Same na Mwanga itainuka.
“Mafanikio ya ukamilishaji wa mradi huu ni muhimu sana kwa uchumi wa jamii na maisha bora kwa watu wa wilaya ya Same na Mwanga”. Alisema Likwelile.
Dr. Likwelilie alimalizia kwa kusema kuwa“Tanzania na Saudia ni marafiki wa muda mrefu sana, hivyo tutazidi kushirikiana na kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa”. 
Hali ya hewa ya mjini Washington Dc. ni mvua za vipindi na baridi kiasi.
Imetolewa na:
Ingiahedi Mduma
Msemaji - Wizara ya Fedha
Washington D.C
11/10/2014
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dr.    Servacius Likwelile akitia saini makubaliano ya mradi wa maji katika Wilaya ya Same na Mwanga. Aliye kushoto kwake ni Eng. Yousef I. Al-Bassam ambaye ni Makamu wa Mwenyekiti  na Mkurugenzi Msimamizi wa mfuko wa maendeleo wa Saudia. Aliyeko kulia ni Bi. Suzan Mkapa, Mkurugenzi wa sheria kutoka Wizara ya Fedha.

No comments:

Post a Comment