SAFARI YA TAIFA STARS MISRI 2019

HATIMAYE Tanzania itacheza tena Fainali za Kombe la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Juni mwaka huu nchini Misri, baada ya kufuzu kama mshindi wa pili wa Kundi L, nyuma ya Uganda Machi 24, mwaka huu.
Hiyo itakuwa mara ya pili tu Taifa Stars inashiriki AFCON baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria, wakati huo bado michuano hiyo ikijulikana kama Fainali za Kombe la Mataifa Huru ya Afrika. Taifa Stars ilikwenda Lagos baada ya kuzitoa Mauritius na Zambia katika raundi mbili tu za mchujo.
Aprili 16, 1979; Taifa Stars ilifungwa 3-2 na Mauritius 3-2 mjini Curepipe kabla ya kushinda 4-0 kwenye mchezo wa marudiano Aprili 29, 1979 mjini Dar es Salaam.
Agosti 11, 1979; Tanzania ilishinda 1-0 dhidi ya Zambia, bao pekee la kiungo Mohammed ‘Adolph’ Rishard mjini Dar es Salaam kabla ya kwenda kulazimisha sare ya 1-1 na KK Eleven mjini Ndola Agosti 26,  1979 wenyeji wakitangulia kwa bao la Chola dakika ya 43, kabla ya Peter Tino kusawazisha dakika ya 84, hivyo Taifa Stars ikafuzu kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1.
Na kwenye fainali za Lagos 1980 Tanzania ilipangwa Kundi A pamoja na wenyeji, Nigeria, Misri na Ivory Coast na ikatolewa raundi ya kwanza tu enzi hizo makundi mawili tu, timu nane zinashiriki tofuati na sasa 24. 
Machi 8, 1980 ilifungwa 3-1 na Nigeria 3-1 mabao ya wenyeji yakifungwa na Lawal dakika ya 11, Onyedika dakika ya 35 na Odegbami dakika ya 85, huku bao la kufutia machozi la Taifa Stars likifungwa na kiungo Juma Mkambi ‘Jenerali’ (sasa marehemu) dakika ya 54 Uwanja wa Surulere.
Machi 12, 1980; ilifungwa 2-1 Misri, mabao ya washindi yakifungwa na Hassan Shehata dakika ya 32 na Nour dakika ya 38 huku la Taifa Stars likifungwa na Thuweni Ally dakika ya 86.
Machi 15, 1980; Taifa Stars ikahitimisha mechi zake za Kundi A kwa sare ya 1-1 na Ivory Coast waliotangulia kwa bao la Koma dakika ya saba kabla ya Thuweni Ally kuisawazishia Tanzania dakika ya 59.
Kikosi cha Taifa Stars kilichotumika kwenye mechi za kufuzu kiliundwa na makipa; Omar Mahadhi (Simba SC), Juma Pondamali (Pan Africans) na Iddi Pazi (Maji Maji FC).
Mabeki; Leopold ‘Tasso’ Mukebezi (Balimi FC), Mohammed Kajole (Simba SC), Daudi Salum ‘Bruce Lee’ (Simba SC), Ibrahim Kapenta (KMKM), Jellah Mtagwa (Pan Africans), Leodegar Tenga (Pan Africans) na Salim Ameir (Coastal Union).
Viungo; Juma Mkambi (Yanga), Hussein Ngulungu (Tumbaku), Mohammmed Rishard Adolph (Pan Africans), Shaaban Katwila (Yanga SC), Omar Hussein (Yanga SC), Thuweni Ally (Simba), George Kulagwa (Simba SC). 
Washambuliaji; Peter Tino (African Sports), Mohamed Salim (Coastal Union) Shaaban Ramadhani (KMKM). Kocha Mkuu alikuw Ray Gama na Msaidizi wake, Joel Bendera wote.
Na kikosi kilichoshiriki fainali hizo mjini Lagos kiliundwa na makipa; Athumani Mambosasa (Simba SC), Juma Pondamali (Pan Africans) na Iddi Pazi (Maji Maji FC).
Mabeki; Leopold ‘Tasso’ Mukebezi (Balimi FC), Mohammed Kajole (Simba SC), Daudi Salum ‘Bruce Lee’ (Simba SC), Ahmad Amasha (Yanga SC), Leodegar Tenga (Pan Africans), Salim Ameir (Coastal Union) na Rashid Iddi ‘Chama’ (Yanga SC).
Viungo; Juma Mkambi (Yanga), Mtemi Ramadhani (Waziri Mkuu), Hussein Ngulungu (Tumbaku), Mohammed Rishard Adolph (Pan Africans) na Willy Kiango (Mwadui FC).
Washambuliaji; Charles Alberto (KMKM), Omar Hussein (Yanga SC), Peter Tino (African Sports), Mohamed Salim (Coastal Union), Thuweni Ally (Simba SC), Shaaban Ramadhani (KMKM).
Makocha walikuwa Mpoland Slamielk Work na Joel Bendera Msaidizi wake.
Miaka 39 baadaye, Tanzania inafuzu tena AFCON, ambayo imeboreshwa mno na idadi ya timu zimeongezeka kutoka nane hadi 24. Je safari ya Taifa Stars kwenda Misri ilikuwaje? Ungana na mwandishi gwiji wa michezo nchini, Mahmoud Bin Zubeiry kwa makala hii. 
Januari 12, 2017 Tanzania ilipangwa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon pamoja na Uganda, Cape Verde na Lesotho katika droo iliyopangwa usiku huo mjini Libvreville, Gabon.
Hili lilichukuliwa kuwa kundi rahisi zaidi kwa Taifa Stars, kwani zote Uganda, Cape Verde na Lesotho ni timu ambazo zipo ndani ya uwezo wake - kikubwa ni maandalizi ni mshikamano wa Watanzania kama taifa.
Januari 19, 2017; Mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Athumani Machuppa alisema si rahisi Tanzania kufuzu AFCON 2019 kama baadhi wanavyofikiria.
Machuppa anayeishi Sweden kwa sasa, alisema; “Kama tunataka kwenda Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 lazima tujipange haswa,”.
Akifafanua mchezaji huyo wa zamani wa Simba, Al Hemria, Sharjah za Dubai, Atraco FC ya Rwanda, Aalborg FF ya Denmark na Vasalund IF ya Sweden, amesema kujipanga ni kwa maandalizi, kwani viwango vya wapinzani wetu katika Kundi L si vya kubeza.
Machi 13, 2017; Kocha Salum Mayanga akataja kikosi cha kwanza kabisa cha Taifa Stars kwa maandalizi ya mechi za kufuzu AFCON 2019, akiiita wachezaji 26 kambini ambao ni. 
Makipa; Aishi Manula (Azam), Deogratius Munishi ‘Dida’ (Yanga) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar).
Mabeki; Shomary Kapombe (Azam), Hassan Kessy (Yanga), Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ (Simba), Gardiel Michael (Azam), Andrew Vincent (Yanga), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba) na Erasto Nyoni (Azam FC).
Viungo ni Himid Mao (Azam), Jonas Mkude (Simba), Salum Abubakar ‘Sure Boy’ (Azam), Said Ndemla (Simba), Frank Domayo (Azam), Muzamil Yassin (Simba), Simon Msuva (Yanga), Shiza Kichuya (Simba), Farid Mussa (DC Tennerife) na Hassan Kabunda (Mwadui FC).
Washambuliaji ni Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji), Thomas Ulimwengu (AFC Eskilstuna, Sweden), Ibrahim Hajib (Simba), Mbarak Yussuf (Kagera Sugar) na Abdulrahman Mussa (Ruvu Shooting).
Machi 25, 2017; Mabao mawili ya Nahodha Mbwana Ally Samatta yaliipa Taifa Stars ushindi wa 2-0 dhidi ya Botswana katika mchezo wa kujiandaa ne mechi za Kundi L kufuzu AFCON ya 2019 uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Huo ulikuwa mchezo wa kwanza Taifa Stars inacheza chini ya kocha wake mpya, Salum Mayanga aliyerithi mikoba ya Charles Boniface Mkwasa aliyeng’atuka Janauri.
Katika mchezo huo uliodhuhuriwa na Waziri mpya wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk Harison Mwakyembe, Samatta alifunga mabao yake dakika ya pili akimalizia pasi ya Shiza Kichuya na 87 kwa shuti la mpira wa adhabu.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni, Abdi Banda, Himid Mao/Jonas Mkude, Simon Msuva/Said Ndemla, Frank Domayo/Muzamil Yassin, Mbwana Samatta, Ibrahim Hajib na Shiza Kichuya/Farid Mussa. 
Botswana: Kabelo Dambe, Tapiwa Gadibolae, Kaone Vanderwesthuizem, Lesenya  Ramoraka, Lesego Galenamotlhale, Ofentse Nato, Lebogang Ditsele, Omaaatla Kebatho, Mosha Gaolaolwe, Thacng Sesenyi na Mogakolod Ngele.
Machi 28, 2017 Taifa Stars iliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Burundi katika mchezo wa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya Taifa Stars yalifungwa na Simon Happygod Msuva dakika ya 22 na Mbaraka Yussuf Abeid dakika ya 77, wakati la Burundi lilifungwa na mshambuliaji wa Simba SC, Laudit Mavugo dakika ya 53. Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Salim Mbonde, Himid Mao, Muzamil Yassin/Jonas Mkude, Salum Abubakr ‘Sure Boy’/Said Ndemla, Ibrahim Hajib/Shiza Kichuya, Farid Mussa/Mbaraka Yussuf na Simon Msuva. Burundi; Jonathan Nahimana, Gael Duhayindavya, Rashid Harerimana, Omary Moussa, David Nshirimimana/Eric Ndoyirobija, Youssouf Ndayishimiye, Tresor Ndikumana, Jean Ndarusanze/Franck Barirengako, Laudit Mavugo, Kiza Fataki/Moustapha Selemani na Djuma Nzeyimana/Sudi Ntirwaza.
Mei 12, 2017 Kampuni ya Bia ya Serengeti Breweries Limited (SBL) ilitangaza udhamini wa Sh. Bilioni 2.1 kwa miaka mitatu kwa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars katika ukumbi wa Kivukoni 4, hoteli ya Serena, Dar es Salaam.
Hiyo ilikuwa ni mara ya pili kwa SBL kuidhamini timu ya taifa baada ya kampuni hiyo kufanya hivyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia 2008 hadi 2011.
Katika makubaliano hayo ambayo yalisainiwa leo na pande hizo mbili na Mkurugenzi Mkuu wa SBL Helene Weesie na Rais wa TFF Jamal Malinzi, kampuni ya SBL itapata fursa ya kutanga biashara yake wakati wa mechi zote za Taifa Stars za nyumbani na ugenini.
Hafla ya kusainiwa kwa udhamini huo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Dk. Harisson Mwakyembe ambaye  alitoa wito kwa  kampuni zingine na watu binafsi wenye mapenzi na michezo kujitokeza na kutoa michango ya hali na mali ili kuendeleza sekta hiyo.
Mei 31, 2017 KIKOSI cha Taifa Stars imewasili mjini Alexandria nchini Misri kuweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo wa kwanza wa kufuzu AFCON dhidi ya Lesotho utakaofanyika Juni 10, 2017 kwenye Uwanja wa Azam ulioko Chamazi nje kidogo ya jiji la  Dar es Salaam.
Stars iliyokuwa na jumla ya watu 30 wakiwamo viongozi, benchi la ufundi na wachezaji kwa ujumla, ilitua Uwanja wa Ndege ya Cairo, Misri majira ya saa 7.45 usiku ambako mbali ya wenyeji Tolip Sports City, pia ilipokelewa na maofisa wa ubalozi wa Tanzania walioko hapa Misri.
Baada ya kupokelewa, timu hiyo ilisafiri kwa gari maalumu kutoka Cairo, Misri hadi Alexandria umbali wa zaidi ya kilomita 180 na kufika alfajiri baada ya mwendo wa takribani saa mbili. 
Wachezaji wanaounda kikosi hicho cha Kocha Salum Mayanga ni makipa Aishi Manula  (Azam FC), Benno Kakolanya  (Yanga SC) na Said Mohammed (Mtibwa Sugar). 
Walinzi wa pembeni wako Shomari Kapombe    (Azam FC), Hassan Kessy (Yanga SC), Mohammed Hussein (Simba) na Gadiel Michael.
Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Mbonde (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) ilihali viungo wa kuzuia ni Himid Mao (Azam FC) na Jonas Mkude kutoka Simba SC ambaye kwa sasa anapatiwa matibabu baada ya kupata ajali.
Viungo wa kushambulia Salum Abubakar (Azam FC), Said Ndemla  (Simba SC) na Mzamiru Yassin (Simba) wakati viungo wa pembeni ni Simon Msuva (Yanga SC), Shizza Kichuya (Simba SC) na Farid Mussa (Teneriffe, Hispania).
Washambuliaji wapo Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdurahman Mussa (Ruvu Shooting).
Wasaidizi wa Mayanga katika benchi la ufundi ni Novatus Fulgence ambaye ni kocha msaidizi Patrick Mwangata - kocha wa makipa pia yumo Meneja wa timu, Danny Msangi; Mtunza Vifaa, Ally Ruvu, Daktari wa timu ni Richard Yomba na Daktari wa viungo ni Gilbert Kigadye.
Juni 10, 2017 Tanzania ilianza vibaya mbio za kuwania tiketi ya Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 nchini Cameroon baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Lesotho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wa kwanza wa Kundi L.
Sare hiyo inamaanisha kocha Salum Mayanga ameshindwa kuvunja mwiko wa muda mrefu wa Taifa Stars kutoshinda mechi zaidi ya mbili, baada ya kushinda mechi mbili za kirafiki mwezi Machi 2-0 dhidi ya Botswana na 2-1 dhidi ya Burundi.
Katika mchezo wa leo, Tanzania ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 27 kupitia kwa Nahodha wake, Mbwana Ally Samatta kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya beki wa kushoto, Gardiel Michael kuangushwa nje ya boksi. 
Hata hivyo, bao hilo halikudumu, kwani Lesotho, au Mamba walisawazisha dakika ya 34 kupitia kwa Thapelo Tale aliyeunganisha pasi nzuri ya Jane Thaba-Ntso.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Abdi Banda, Salim Mbonde, Himid Mao, Simon Msuva/Farid Mussa dk71, Muzamil Yassin/Salum Abubakar ‘Sure Boy’ dk71, Thomas Ulimwengu, Mbwana/Mbaraka Yussuf dk78, Samatta na Shiza Kichuya.
Lesotho; Likano Mphuti, Mafa Moremoholo, Bokang Sello, Kopano Seka, Thapelo Mokhelo, Bokang Mothoana, Tumelo Khutlang/Mabuti Potloane dk61, Tsoanelo Koetle, Taphelo Talle, Hlompho Kaleko na Jane Thaba Ntso.
Juni 11, 2017 MSHAMBULIAJI wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Athumani Machuppa aliishauri TFF itafute kocha wa kiwango cha juu kwa ajili ya timu ya taifa, Taifa Stars, kwani Salum Mayanga peke yake hawezi. 
Ushauri huo wa mchezaji huyo wa zamani wa Simba ya nyumbani na Vasalunds IF ya Sweden, ulifuatia Taifa Stars kulazimishwa sare ya 1-1 na Mamba wa Lesotho katika mchezo wa kwanza wa Kundi L kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2019 Cameroon.
Juni 25, 2017 Tanzania ilianza vyema michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) baada ya ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa Kundi A dhidi ya Malawi jioni ya leo Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
Shukrani kwake winga wa Simba SC ya nyumbani, Shiza Ramadhani Kichuya aliyefungua vizuri akaunti yake ya mabao Taifa Stars kwa kufunga mabao yote hayo kipindi cha kwanza, dakika ya 13 na 18.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe/Hassan Kessy, Gardiel Michael, Abdi Banda, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Himid Mao, Shiza Kichuya, Simon Msuva, Muzamil Yasssin, Elias Maguri/Mbaraka Yussuf dk62.
Juni 27, 2017 Kiungo wa Simba, Muzamil Yassin Said aliibuka mchezaji Bora wa mechi ya pili ya Kundi A, Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika, COSAFA Castle 2017, Tanzania ikitoa sare ya 0-0 na Angola Uwanja wa Royal Bafokeng mjini Rusternburg, Afrika Kusini usiku wa leo.
Kikosi cha Tanzania leo kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Salim Mbonde, Abdi Banda, Himid Mao, Erasto Nyoni, Simon Msuva/Mbaraka Yussuf dk68, Muzamil Yassin, Elias Maguri/Stahmili Mbonde dk89 na Shiza Kichuya/Thomas Ulimwengu dk74.
Angola; Gerson Barros, Lunguinha, Wilson, Dani Masunguna, Natael/To Carneiro dk23, Paty, Herenilson, Dudu Leite, Nelson, Caporal na Amaro/Carlinhos dk76.
Juni 29, 2017 Tanzania ilikwenda Robo Fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Kusini mwa Afrika (COSAFA) Castle baada ya sare ya 1-1 na Mauritius jioni ya leo Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
Pongezi kwake winga Simon Happygod Msuva aliyetokea benchi kipindi cha pili na kwenda kuifungia Taifa Stars bao la kusawazisha dakika ya 68, dakika moja tu baada ya Kevin Perticots aliyetokea benchi pia kuifungia bao la kuongoza Mauritius.
Kwa matokeo hayo, Tanzania itamenyana na wenyeji, Afrika Kusini 'Bafana Bafana' Jumapili Uwanja wa Royal Bafokeng Sports Palace katika Robo Fainali.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Abdi Banda, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Himid Mao, Shiza Kichuya, Elias Maguri/Simon Msuva dk58 na Thomas Ulimwengu.
Mauritius; K. Jean-Louis, M. Dorza, E. Vincent-Jean, D. Balisson, C. Bell, L. Rose, A. Langue/J.Jocelyn dk87, L. Rungassamy/K. Perticots dk46, J. Villeneuve, W. St Martin/K. Saramandif dk77 na F. Rasolofonirina.
Julai 2, 2017 BAO pekee la mshambuliaji Elias Maguri lilitosha kuipeleka Tanzania Nusu Fainali ya michuano ya Kombe la COSAFA Castle baada ya kuwalaza wenyeji, Afrika Kusini 1-0 Uwanja wa Royal Bafokeng, Rusternburg.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Olivio Saimone wa Msumbiji aliyesaidiwa na Matheus Kanyanga wa Namibia na Jackson Pavaza wa Namibia, Maguri alifunga bao hilo dakika ya 18 kwa shuti la mahesabu baada ya pasi ndefu ya kiungo Muzamil Yassin, Stars ikitoka kushambuliwa.
Tanzania sasa itamenyana na Zambia Jumatano katika Nusu Fainali, wakati Afrika Kusini wanaangukia kwenye michuano ya Plate, inayohusisha timu zilizotolewa hatua ya Robo Fainali.
Kikosi cha Afrika Kusini; Boalefa Pule, Thendo Mukumela, Innocent Maela, Lorenzo Gordinho, Mario Booysen, Lehlogonolo Masalesa, Cole Alexander, Riyaad Norodien/Lebogang Maboe dk77, Jamie Webber, Liam Jordan na Judas Moseamedi/Mohau Mokate dk60.
Tanzania; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Himid Mao, Muzamil Yassin, Raphael Daudi/Salmi Hoza dk89, Thomas Ulimwengu/Msuva dk49, Elias Maguri na Shiza Kichuya/Hamim Karim dk90.
Julai 5, 2017 Tanzania ilifungwa mabao 4-2 na Zambia katika mchezo wa Nusu Fainali Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
Zambia inatangulia fainali na Julai 9 itamenyana na mshindi kati ya Lesotho na Zimbabwe zinazomenyana kuanzia Saa 2:00 usiku wa leo, wakati Tanzania itawania nafasi ya tatu dhidi ya Lesotho.
Mkongwe Erasto Nyoni alianza kuifungia Taifa Stars kwa shuti zuri la mpira wa adhabu dakika ya 14 na bao hilo lilikaribia kudumu hadi kipindi cha pili, kama si Zambia kupata mabao mawili ya haraka haraka mwishoni mwa kipindi hicho.
Justin Shonga wa Zambia akimtoka beki wa Tanzania, Abdi Banda leo Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini
Brian Mwila alianza kuifungia Chipolopolo bao la kusawazisha dakika yaa 44, kabla ya Justin Shonga kufunga la pili dakika ya 45 na Zambia ikaenda kupumzika inaongoza 2-1.
Jackson Chirwa akaifungia Zambia bao la tatu kwa mkwaju wa penalti dakika ya 55, baada ya mpira kumgonga mkononi kwa nyuma beki wa kushoto, Gardiel Michael na la nne dakika 67 kwa shuti la mpira wa adhabu.
Simon Msuva akaipunguzia machungu Tanzania kwa kufunga bao la pili dakika ya 84 akimalizia mpira uliorudi baada yaa krosi ya Gardiel Michael.  Taifa Stars wakaongeza kasi ya mashambulizi baada ya bao hilo, lakini bahati mbaya ‘muda haukuruhusu’. 
Taifa Stars ilipoteza mechi ya kwanza chini ya kocha Salum Mayanga aliyeanza kazi Machi mwaka 2017 akimpokea Charles Boniface Mkwasa, baada ya kucheza mechi saba bila kupoteza, ikishinda tatu na kutoa sare nne. 
Tanzania ilianzia hatua ya mchujo kwenye Kundi A ambako iliongoza kwa pointi zake tano sawa na Angola baada ya sare mbili 0-0 na Angola, 1-1 na Mauritius na ushindi wa 2-0 dhidi ya Malawi, hivyo kutengeneza wastani mzuri wa mabao na kuwapiku wapinzani kusonga Nusu Fainali.
Zambia yenyewe ilianzia moja kwa moja hatua ya Robo Fainali sawa na Afrika Kusini, Botswana, Namibia, Lesotho na Swaziland huku Zimbabwe ikiongoza Kundi B. 
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Abdi Banda/Nurdin Chona dk69, Salim Mbonde, Himid Mao, Erasto Nyoni/Raphael Daudi dk45, Muamil Yassin, Elias Maguri/Thomas Ulimwengu dk80, Simon Msuva na Shiza Kichuya.
Zambia; Alan Chibwe, Lawrence Chungu, Adrian Chama, Diamond Chikwekwe/Lubinda Mundia dk61, Justin Shonga/Godfrey Ngwenya dk90, Donashano Malama, Mike Katiba, Jackson Chirwa, Webster Mulenga, Isaac Shamujompa na Brian Mwila/Chitia Mususu dk82.  
Julai 7, 2017 Tanzania ilifanikiwa kushika nafasi ya tatu katika michuano ya COSAFA Castle baada ya ushindi wa penalti 4-2 dhidi ya Lesotho kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku huu Uwanja wa Moruleng mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
Shujaa wa Taifa Stars siku hiyo alikuwa golikipa Said Mohammed Mduda aliyepangua penalti ya Nahodha wa Mamba, Thapelo Mokhehle baada ya Sera Motebang kugongesha mwamba wa kulia mkwaju wake na kurudi uwanjani.
Waliofunga penalti za Lesotho ni Hlompho Kalake na Tsoanelo Koetle wakati Shiza Kichuya aligongesha mwamba wa juu penalti ya kwanza ya Tanzania, kabla ya Nahodha Himid Mao,Simon Msuva, Abdi Banda na Raphael Daudi kumtungua kipa wa Mamba Samuel Ketsekile kuipatia Taifa Stars ushindi mzuri wa 4-2.
Ushindi ulikuja siku 25 baada ya timu hizo kutoka sare ya 1-1 Juni 10, mwaka huo katika mchezo wa ufunguzi wa Kundi L kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Kutoka na ushindi huo, Tanzania inaondoka na dola za Kimarekani 10,000 zaidi ya Sh. Milioni 22 kwa fedha za nyumbani, wakati Lesotho wamepata dola 8,300.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Said Mohammed, Shomary Kapombe, Gardiel Michael, Nurdin Chona, Salim Mbonde/Abdi Banda dk61, Salmin Hoza/Muzamil Yassin dk61, Himid Mao, Simon Msuva, Raphael Daudi, Stahmili Mbonde/Elias Maguri dk71 na Shiza Kichuya.
Lesotho; Samuel Ketsekile, Itumeleng Falene, Motlomelo Mkwanazi, Thapelo Mokhehle, Bokang Sello, Kefuce Mahula/ Hlompho Kalake dk89, Tumelo Khutlang, Tsoanelo Koetle, Napo Matsoso, Jane Ntso/ Mabuti Potloane dk59 na Sera Motebang.
Julai 15, 2017 Tanzania ikaanza vibaya kampeni za kuwania tiketi ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza nchini mwao pekee, baada ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Rwanda katika mchezo wa kwanza wa raundi ya kwanza ya mtoano.
Dominique Savio Nshuti alianza kuifungia Amavubi dakika ya Dk 17 akiitelezea krosi ya Emmanuel Imanishimwe, kabla ya Nahodha Himid Mao Mkami ‘Ninja’ kuisawazisha Tanzania dakika ya 34 kwa penalti baada ya Rucogoza Aimable kuunawa mpira uliopigwa na beki Gardiel Michael.
Kikosi cha Tanzania kilikwa; Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Nurdin Chona, Salim Mbonde, Erasto Nyoni, Simon Msuva, Himid Mao, John Bocco/Stahmili Mbonde dk93, Muzamil Yassin na Shiza Kichuya.
Rwanda; Ndayishimiye Eric, Marcel Mubumbyi/Latif Bishira dk63, Bizimana Djihad, Dominique Savio Nshuti/Innocent Nshuti dk94, Emmanuel Imanishimwe, Iradukunda Eric, Manzi Thierry, Mico Juastin/Kayumba Soter dk81, Yannick Mukunzi, Nsabimane Aimable na Rucogoza Aimable.
Julai 22, 2017  Tanzania ikaondolewa mapema kwenye kinyang’anyiro cha tiketi ya CHAN, baada ya kulazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji Rwanda Uwanja wa Kigali, uliopo Nyamirambo mjini Kigali.
Kikosi cha Rwanda kilikuwa; Ndayishimiye Eric, Rucogoza Aimable, Nsabimana Aimable, Yanick mukunzi, Kevin Muhire/Latif Bishira dk67, Mico Justin, Thierry Manzi, Eric Iradukunda, Emmanuel Imanishimwe, Dominique Savio Nshuti/Kayumba Soter dk 91 na Djihad Bizimana.
Tanzania; Aishi Manula, Boniphace Maganga, Gardiel Michael, Erasto Nyoni, Salim Mbonde, Himid Mao, Simon Msuva/Joseph Mahundi dk66, Muzamil Yassin, John Bocco ‘Adebayor’, Raphael Daudi/Said Ndemla dk 62 na Shiza Kichuya.
Agosti 12, 2017;  Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilipata uongozi mpya chini ya Rais, Wallace Karia katika uchaguzi uliofanyika ukumbi wa mikutano wa jengo la St. Gasper mjini Dodoma.
Karia aliwashinda mchezaji wa zamani wa Taifa Stars, Ally Mayay, Katibu wa zamani wa shirikisho hilo, Frederick Mwakalebela, Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Yanga, Wakili Imani Madega, Mwandishi wa Habari za Michezo wa zamani, Shija Richard na Katibu wa klabu ya Mbeya City, Emmanuel Kimbe.
Michael Richard Wambura alishinda nafasi ya Umakamu wa Rais akiwaangusha Mwenyekiti wa FA ya Dodoma, Mulamu Nghambi, mchezaji wa zamani wa timu ya taifa, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.
Karia alipata kura 95 kati ya 125 zilizopigwa, akifuatiwa na Mayay na Shija  waliopata kura 9 kila mmoja,  huku Wambura akipata kura 85 kati ya 125, akifuatiwa na Mulamu Nghambi aliyepata kura 25.
Wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshinda ni Lameck Nyambaya kutoka Kanda ya Dar es Salaam aliyepata kura 41, akifuatiwa na Shaffi Dauda aliyepata kura 21, Khaled Mohammed kwa Kanda ya Kilimanjaro na Tanga aliyepata kura 70 na Fransis Ndulami kura 7O Kanda ya Pwani na Morogoro.
Wengine ni Mohamed Ally 35 kanda ya Dodoma na Singida, Dunstan Ditopile kura 74 Kanda ya Lindi na Mtwara, James Mhagama kura 63 Njombe na Ruvuma, Elius Mwanjala kura 61 Mbeya na Ruvuma, Kenneth Pesambili 72 Katavi na Rukwa, Issa Bukuku kura 80 Kigoma na Tabora, Sara Chau kura 57 Manyara na Arusha, Mbasha Matutu kura 67 Shinyanga na Simiyu, Modestus  Lufanga kura 67 Mara na Mwanza, Salim Chama kura 92 Kagera na Geita.
Baada ya matokeo hayo, washindi wote wa waliapishwa kwa agizo la Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe
Ikumbukwe aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi alishindwa kurudi kutetea nafasi yake baada ya kuweka rumande tangu Juni 29, mwaka huu kwa pamoja na Katibu weke, Selestine Mwesigwa na Isinde Isawafo Mwanga kwa tuhuma za ubadhirifu.
Watatu hao walipelekwa rumande Juni 29 baada ya kusomewa mashitaka 28 ya kughushi na kutakatisha fedha kupitia akaunti ya TFF iliyopo katika banki ya Stanbic, Dar es Salaam.
Katika mashitaka hayo, 25 yanakwenda moja kwa moja kwa Rais wa shirikisho hilo, Malinzi akidaiwa kughushi michakato mbalimbali ya kifedha, huku matatu yakiwahusu wote na Katibu wake na Mhasibu wake Nsiande Isawafo Mwanga.
Malinzi aliingia madarakani TFF Oktoba mwaka 2013 baada ya kupata kura 72 kati ya 126 zilizopigwa akimshinda aliyekuwa mpinzani wake wa karibu, Athumani Nyamlani, lakini baada ya kesi hiyo kuanza kuunguurma na kuwekwa rumande, Kamati ya Utendaji ya TFF ilikutana na kumteua Makamu wake, Wallace Karia kukaimu Urais wa shirikisho hilo.
Septemba 2, 2017 Mabao mawili ya winga mpya wa klabu ya Difaa Hassan El- Jadida, Simon Msuva yaliipa Tanzania ushindi wa 2-0 dhidi ya Botswana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kevin Yondan, Himid Mao, Simon Msuva/Emmanuel Martin dk82, Hamisi Abdallah/Said Ndemla dk80, Muzamil Yassin/Raphael Daudi dk57, Mbwana Samatta/Elias Maguri dk82 na Shiza Kichuya/Farid Mussa dk66.
Botswana; Mwambule Masule, Mosha Gaolaolwe/Jackson Lesole dk74, Edwin Olerile/Tmisang Orebonye7 dk4, Simisami Mathumo, Lopang Mogise, Alphonce Modisaotsile, Maano Ditshupo/Katlego Masole dk70, Gift Moyo, Segolame Boy, Kabelo Seakanyeng na Ontireste Ramatlhakwana.
Oktoba 7, 2017 Taifa Stars pamoja na kucheza pungufu ya wachezaji wawili, viungo Erasto Nyoni na Muzamil Yassin kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi cha pili ilitoa sare ya 1-1 na Malawi katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Israel Mujuni Nkongo aliyeisaidiwa na Frank Komba na Soud Lila wote wa nyumbani, Malawi walitangulia kwa bao la Nahodha wake, Robert Ng’ambi dakika ya 35 kwa kichwa , kabla ya Simon Msuva kuisawazishia Taifa Stars dakika ya 57 kwa kona iliyoingia moja kwa moja.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Abdi Banda, Kevin Yondan, Himid Mao, Simon Msuva/Adul Hilal dk85, Hamisi Abdallah/Muzamil Yassin dk14, Mbwana Samatta, Raphael Daudi/Mbaraka Yussuf dk54 na Shiza Kichuya/Ibrahim Hajib dk58.
Malawi; Swini Charles, Gomezgan Chirwa, Lanjesi John, Chambezi Denis, Fodya Nyamkuni, Ngambi Robert, Phiri Gerald, Banda John/Bandawe Fretcher, Chirwa Chikoti, Mhango Gabadinho na Mbulu Richard.
Novemba 12, 2017 Taifa Stars ililazimisha sare ya kufungana bao 1-1 na wenyeji, Benin katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa l'Amitie, au Urafiki mjini Cotonou.
Benin walitangulia kwa bao la penalti la mkongwe na Nahodha wake, Stephane Sessegnon dakika ya 33, kabla ya Elias Maguri kuisawazishia Tanzania dakika ya 50.
Kikosi cha Benin kilikuwa; Fabien Farnole, Rodrigue Fassinou, Khaled Adenon, Cedric Hountonji, David Kiki, Djiman Koukou, Olivier Verdon, Jodel Dossou, Stephane Sessegnon, David Djigla Dossou na Steve Mounie.  
Tanzania; Aishi Manula, Himid Mao, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondan, Hamisi Abdallah/Jonas Mkude dk75, Simon Msuva/Boniphace Maganga dk85, Mudathir Yahya/Nurdin Chona dk92, Elias Maguli, Raphael Daudi/Mbaraka Yusuph dk54 na Shizza Kichuya/Ibrahim Ajib dk65.
Machi 22, 2018 Taifa Stars ikapunguza unyonge kwa Algeria, baada ya kufungwa mabao 4-1 katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Julai 5, 1962 mjini Algiers kutoka kufungwa 7-0  Novemba 17, mwaka 2015 katika mchezo wa kufuzu Kombe la Dunia.
Siku hiyo kipa Ally Mustafa Barthez alifungwa mabao matatu kipindi cha kwanza na kipindi cha pili akaingia Aishi Manula naye akapigwa nne Uwanja wa Mustapha Tchaker mjini Blida, kiungo Mudathir Yahya akitolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 41, baada ya njano ya kwanza dakika ya 22. 
Siku hiyo, mabao ya Algeria yalifungwa na Yacine Brahimi dakika ya kwanza, Faouzi Ghoulam mawili dakika ya 23 na 59 kwa penalti, Ryad Mahrez dakika ya 43, Islam Slimani mawili moja kwa penalti dakika ya 49 na lingine dakika ya 75 na Carl Medjani dakika ya 72.
Na Machi 22, 2018 tena Carl Medjani alifunga moja, wakati mabao mengine yalifungwa na Baghdad Bounedjah mawili na Shomari Kapombe aliyejifunga huku bao la Taifa Stars likifungwa na winga Simon Msuva.
Kikosi cha Algeria kilikuwa; Faouzi Chaouchi, Carl Medjani, Aissa Mandi, Ramy Bensebaini/ Farouk Chafaï dk68, Sofiane Hanni/Mohamed Lamine Abid dk83, Riyad Mahrez, Zinedine Ferhat, Nabil Bentaleb/ Ismael/Bennacer dk60, Salim Boukhanchouche/ Farid El Melali dk89, Hillel El Arbi Soudani/ Mokhtar Benmoussa dk78 na Baghdad Bounedjah.
Tanzania; Abdulrahman Mohamed, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondani, Mudathir Yahya, Said Ndemla/Erasto Nyoni dk62, Himid Mao, Mbwana Samatta, Simon Msuva/Rashid Mandawa dk89 na Shiza Kichuya/Mohammed Issa ‘Banka’ dk74.
Desemba 6, 2017 Kocha aliyeiwezesha Tanzania kufuzu fainali pekee za Kombe la soka la Mataifa ya Afrika (AFCON), Joel Nkaya Bendera amefariki dunia jioni ya leo katika hospitali ya taifa ya Muhimbili Jijini Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu. 
Machi 27, 2018 Tanzania ikaonyesha inaweza baada ya kuifunga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) mabao 2-0 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, mabao ya Nahodha Mbwana Ally Samatta na Shiza Ramadhani Kichuya, huo ukiwa ushindi wa kwanza Taifa Stars tangu Julai 7 mwaka 2017 ilipoichapa kwa matuta Lesotho baada ya sare ya 0-0 kwenye Kombe la COSAFA mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Tanzania: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Abdi Banda, Kelvin Yondan, Himid Mao/Mudathir Yahya dk73, Mohammed Issa ‘Banka’/Ibrahim Ajib dk59, Erasto Nyoni, Mbwana Samatta, Simon Msuva/Yahya Zayed dk90 na Shiza Kichuya/Rashid Mandawa dk87. 
DRC; Ley Matampi, Issam Mpeko, Glody Ngoda, Yannick Bangala, Wilfred Moke, Aaron Tshibola/Lema Mabibi dk46, Chancel Mbemba, Mubele Ndombe/Junior Kabananga dk54, Needkens Kebano, Bennick Afobe/Assombalanga Britt dk63 na Yannick Bolasie.
Juni 4, 2018 Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Ally Samatta aliamua kukusanya maoni juu ya namna ya kufanya timu hiyo ifuzu AFCON ya mwaka huu ambayo awali ilikuwa ifanyike nchini Cameroon.
Samatta aliposti ujumbe; “Hivi ukipata nafasi ya kushauri chochote ambacho kinaweza kuifanya 'taifa stars'kupata tiketi ya afcon mwakani unadhan ungeshauri jambo gani? Nini kifanyike? Sina maana ushauri utafatwa ama la lakini tuongelee tu hili jambo hapa,”.
Agosti 6, 2018 Rais wa TFF, Wallace Karia alimtambulisha winga wa zamani wa kimataifa wa Nigeria, Emmanuel Amunike kuwa kocha mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars katika mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika hoteli ya New Africa mjini Dar es Salaam baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili.
Amunike aliyeng’ara na Super Eagles katika fainali za Kombe la Dunia mwaka 1994 nchini Marekani akicheza wingi ya kushoto, aliikuta timu imekwishacheza mechi moja ya kufuzu ya AFCON 2019 na kulazimishwa sare ya 1-1 nyumbani na Lesotho Juni 10, mwaka 2017 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam ikiwa chini ya kocha mzalendo, Salum Mayanga.
Mayanga aliiongoza Taifa Stars kwa mara ya mwisho Machi 27, mwaka 2018 ikishinda 2-0 dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mchezo wa kirafiki Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam.
Siku hiyo, mabao ya Tanzania yalifungwa na Nahodha Mbwana Ally Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji na Shiza Ramadhani Kichuya wa Simba ya nyumbani yanayoipa ushindi wa kwanza Tanzania tangu Julai 7 mwaka jana ilipoichapa kwa matuta Lesotho baada ya sare ya 0-0 kwenye Kombe la COSAFA mjini Rusternburg, Afrika Kusini.
Taifa Stars ikawa timu ya kwanza ya taifa ya wakubwa Amunike kufundisha, baada ya awali kuwa kocha wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya kwao, Nigeria kuanzia mwaka 2014 hadi 2017.
Zaidi ya hapo, Amunike mwenye umri wa miaka 47 amefundisha klabu za Al Hazm ya Saudi Arabia, kama Kocha Msaidizi mwaka 2008 kabla ya kuhamia Julius Berger hadi mwaka 2011 alipojiunga na Ocean Boys, zote za Nigeria.
Alipoachana na U-17 ya Nigeria akaenda kufundisha Al Khartoum SC ya Sudan kuanzia mwaka 2017 hadi 2018 na sasa anakuja kuujaribu ‘mfupa’ uliowashinda wengi, Taifa Stars.   
Kisoka, Amunike aliibukia klabu ya Concord mwaka 1990 kabla ya kwenda kuchezea Julius Berger 1991, zote za kwao, Nigeria baadaye Zamalek ya Misiri mwaka 1991 hadi 1994 ndipo akahamia Ulaya.
Alianza na klabu ya Sporting CP ya Ureno kuanzia 1994 hadi 1996 kabla ya kuhamia Barcelona ambako alicheza hadi mwaka 2000 alipohamia Albacete zote za Hispania na mwaka 2003 alijiunga na Busan I'Cons ya Korea Kusini alikocheza hadi 2004 akahamia Al-Wehdat ya Jordan kumalizia soka yake.
Agosti 29, 2018 wachezaji sita wa Simba SC, mabeki Shomari Kapombe, Erasto Nyoni, viungo Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Hassan Dilunga na mshambuliaji na Nahodha, John Bocco walienguliwa kwenye kikosi cha Taifa Stars kuelekea mechi na Uganda Septemba 8, kwa utovu wa nidhamu. 
Kocha Mnigeria, Emmanuel Amunike alichukua hatua hiyo baada ya wachezaji hao pamoja na kiungo Feisal Salum wa Yanga SC kwa kushindwa kuripoti kambini jana yake, hoteli ya Sea Scape, eneo la Kunduchi mjini Dar es Salaam bila taarifa yoyote, huku mwenzao, kipa, Aishi Salum Manula wa Simba pekee akiripoti.
Agosti 31, 2018 Kocha Emmanuel Amunike aliwasamehe wachezaji sita wa Simba SC waliokaidi kuripoti kambini kwa maandalizi ya mchezo dhidi ya Uganda, baada ya kikao cha pamoja kati ya klabu yao, TFF lakini akataa kuwarejesha kambini kwa ajili ya mchezo huo.
Septemba 8, 2018 Taifa Stars ililazimisha sare ya 0-0 na wenyeji, mjini Kampala huku Nahodha Samatta akipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 70 baada ya kupewa pasi nzuri na Ulimwengu, lakini akiwa akiwa amebaki na kipa Onyango akashindwa kufunga. 
Mpira wa kwanza aliopiga ulimbabatiza kipa huyo lakini ukamrudia na badala ya kutoa pasi kwa wenzake waliokuwa kwenye nafasi, akajaribu kumpiga chenga Onyango akaunasa.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael/Farid Mussa dk71, Aggrey Morris, David Mwantika, Abdi Banda, Simon Msuva, Mudathir Yahya, Mbwana Samatta, Frank Domayo/Himid Mao dk77 na Thomas Ulimwengu/Shaaban Iddi dk90.
KIKOSI KILICHOITWA; Makipa watatu Aishi Manula wa Simba SC, Mohammed Abdulrahman Wawesha wa JKU, Benno Kakolanya wa Yanga SC.
Mabeki ni Shomari Kapombe (Simba SC), Hassan Kessy (Nkana FC, Zambia), Gardiel Michael (Yanga SC), Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Kelvin Yondan (Yanga SC), Aggrey Morris (Azam FC) na Andrew Vincent ‘Dante’ (Yanga SC).
Viungo ni Himid Mao (Petrojet FC, Misri), Mudathir Yahya (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Erasto Nyoni (Simba SC), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadida, Morocco), Shiza Kichuya (Simba SC), Farid Mussa (CD Tenerife, Hispania), Feisal Salum (Yanga SC) na Hassan Dilunga (Simba SC).
Washambuliaji ni Rashid Mandawa (BDF XI, Botswana), Yahya Zayed (Azam FC), Shaaban Iddi Chilunda (CD Tenerife, Hispania), John Bocco (Simba SC), Emmanuel Ulimwengu (El HIlal, Sudan) na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji). 
Oktoba 7, 2018 Mtangazaji wa Redio (RTD) aliyetangaza mchezo kati ya Zambia na Tanzania mjini Ndola Taifa Stars ikitoasare ya 1-1 na kufuzu AFCON ya Lagos, Ahmed Jongo alifariki dunia katika hospitali ya Temeke mjini Dar es Salaam.    
Oktoba 9, 2018 kocha Emmanuel Amunike aliongeza makipa wawili, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons na Benedicto Tinocco wa Mtibwa Sugar katika kikosi kilichokwenda Cape Verde huku akiwaacha kipa Mohammed Abdulrahman wa JKT Tanzania, beki Andrew Vincent ‘Dante na viungo Jonas Mkude na Frank Domayo kwa sababu wote ni majeruhi, wakati kiungo Salum Kihimbwa na mshambuliaji Kelvin Sabato waliachwa kwa sababu za kiufundi.
Oktoba 10, 2018 gwiji wa soka Tanzania, Augustino Peter Magali ‘Peter Tino’ alisafiri na timu ya taifa kwenda mjini Praia nchini Cape Verde.
Oktoba 12, 2018 Taifa Stars ilichapwa 3-0 na wenyeji, Cape Verde mjini Praia, mabao ya Ricardo Jorge Pires Gomes mawili na beki Ianique dos Santos Tavares ‘Stopira’.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael/Shomari Kapombe dk38, David Mwantika/Ally Sonso dk72, Abdi Banda, Aggrey Morris, Himid Mao, Mudathir Yahya/John Bocco dk78, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu na Simon Msuva.
KIKOSI KILICHOITWA; Makipa; Aishi Manula (Simba SC), Beno Kakolanya (Yanga SC) na Mohamed Abdulahman (JKT Tanzania).
Mabeki; Hassan Kessy (Nkana FC/Zambia), Shomari Kapombe (Simba SC), Salum Kimenya (Tanzania Prisons), Gardiel Michael (Yanga SC), Paulo Ngalema (Lipuli FC), Ally Sonso (Lipuli FC), Aggrey Morris (Azam FC), David Mwantika (Azam FC), Abdallah Kheri (Azam FC), Kelvin Yondani (Yanga SC), Andrew Vicent (Yanga SC) na Abdi Banda (Baroka FC).
Viungo ni Himid Mao (Petrojet/Misri), Simon Msuva (Difaa Hassan El –Jadida/Morocco), Mudathir Yahya (Yanga SC), Frank Domayo (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Feisal Salum (Yanga SC), Salum Kihimbwa (Mtibwa Sugar) na Farid Mussa (CD Tenerife/Hispania).
Washambuliaji; Mbwana Samatta (Nahodha, KRC Genk/Ubelgiji), Thomas Ulimwemgu (Al Hilal/Sudan), John Bocco (Simba SC), Yahya Zayd (Azam), Kelvin Sabato (Mtibwa Sugar), Rashid Mandawa (BDF XI/Botswana) na Shaaban Iddi Chilunda (CD Tenerife/Hispania). 
Oktoba 14, 2018 kocha Emmanuel Amunike alimrejesha kikosini beki mkongwe, Erasto Edward Nyoni anayeweza kucheza kama kiungo kuelekea mchezo wa marudiano na Cape Verde kufuatia beki wa kulia, Hassan Kessy ambaye kuwa anatumikia adhabu ya jadi za njano. 
Oktoba 16, 2018 Taifa Stars ilishinda 2-0 dhidi ya Cape Verde Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya Simon Msuva dakika ya 29 na Nahodha Mbwana Samatta dakika ya 58 na kufufua matumaini ya kwenda Misiri.
Mapema dakika ya 22 Nahodha Samatta anayechezea KRC Genk ya Ubelgiji aligongesha mwamba wa juu mkwaju wa penalti uliotolewa na refa Michael Gasingwa wa Rwanda baada ya beki wa MOL Vidi FC ya Hungary Ianique dos Santos Tavares ‘Stopira’ kumuangusha Msuva kwenye boksi.
Kikosi cha Taifa Stars kilikuwa: Aishi Manula, Shomari Kapombe, Gardiel Michael, Aggrey Morris, Abdi Banda/John Bocco dk51, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Himid Mao, Mudathir Yahya/Feisal Salum dk58, Mbwana Samatta/Rashid Mandawa dk89 na Simon Msuva. 
Oktoba 19, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli alikutana na wachezaji Ikulu na kutoa Sh. Milioni 50 kusaidia maandalizi ya mchezo dhidi ya Lesotho na Novemba 6 timu ikaenda kambini Afrika Kusini.
Novemba 14, 2018 Shomari Kapombe aliumia mazoezini katika kambi ya Bloemfontein, Afrika Kusini na akaukosa mchezo dhidi ya Lesotho Novemba 18.
Novemba 18, 2018; Tanzania ilichapwa 1-0 na wenyeji, Lesotho bao pekee la beki wa klabu ya Matlama Maseru, Nkau Lerotholi dakika ya 76 na kutia kiza safari yake ya Misri 2019.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Abdallah Kheri/John Bocco dk83, Ally Sonso, Aggrey Morris, Kelvin Yondan, Erasto Nyoni, Mudathir Yahya/Feisal Salum ‘Fei Toto’dk73, Himid Mao, Simon Msuva, Shaaban Iddi Chilunda na Gardiel Michael/Shiza Kichuya dk59.
KIKOSI KILICHOITWA; Makipa ni; Aishi Manula wa Simba SC, Aaron Kalambo wa Tanzania Prisons, Beno Kakolanya wa Yanga SC na Benedictor Tinocco wa Mtibwa Sugar zote za nyumbani.     
Mabeki ni; Hassan Kessy wa Nkana FC ya Zambia, Abdi Banda wa Baroka FC ya Afrika Kusini, Shomary Kapombe, Erasto Nyoni wa Simba SC, Ally ‘Sonso’ Abdulkarim wa Lipuli FC, Kelvin Yondan, Gardiel Michael wa Yanga SC, Aggrey Morris na Abdallah Kheri wa Azam FC, zoyte za nyumbani.
Viungo ni Himid Mao wa Petrojet ya Misri, Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadidi ya Morocco, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Mudathir Yahya wa Azam FC, Salum KImenya wa Tanzania Prisons, Feisal Salum wa Yanga SC, Jonas Mkude na Shiza Kichuya wa Simba SC zote za nyumbani.
Washambuliaji ni Nahodha Samatta wa KRC Genk ya Ubelgiji, Thomas Ulimwengu wa Al Hilal ya Sudan, Shaaban Iddi Chilunda wa CD Tenerife ya Hispania, Rashid Mandawa wa BDF XI ya Botswana, John Bocco wa Simba SC na Yahya Zayed wa Azam FC zote za nyumbani.
Desemba 24, 2018 Rajab Hassan ‘Kessy’ Rajab alifariki dunia baada ya kupoteza fahamu akitazama mchezo wa Simba na Nkana akiwa Meneja Msaidizi wa Taifa Stars.
Februari 20, 2019; TFF ilitaja Kamati maalum ya watu 14 kwa ajili ya kuisaidia Taifa Stars ifuzu Fainali za AFCON zitakazofanyika kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 mwaka huu nchini Misri chini ya Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Katibu, Mhandisi Hersi Said.
Wajumbe wa Kamati hiyo ni wafanyabiashara Mohamed ‘Mo’ Dewji, Farouk Baghodha, Salum Abdallah ‘Try Again’, Mohammed Nassor, Patrick Kahemele, Abdallah Bin Kleb, Teddy Mapunda, Philemon Ntahilaja, Farid Nahid na Faraji Asas.
Machi 17, 2019; Taifa Stars ikaingia kambini hoteli ya Bahari Beach iliyopo Kunduchi mjini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa mwisho wa Kundi L kufuzu AFCON 2019 dhidi ya Uganda, huku beki Andrew Vincent ‘Dante’ wa Yanga SC akiondolewa na kuongezwa Erasto Edward Nyoni wa Simba SC.
Hoteli ya Bahari Beach ndiyo ilikuwa kambi ya Taifa Stars wakati inafuzu Fainali zake za kwanza za AFCON mwaka 1980 nchini Nigeria.
Machi 21, 2019; Mwenyekiti wa Kamati ya Saida Taifa Stars Ishinde, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda akamtangaza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi katika mchezo dhidi ya Uganda.
Machi 23, 2019; Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akatembelea kambi ya Taifa Stars hoteli ya Bahari Beach mjini Dar es Salaam huku ahadi ikitolewa iwapo Tanzania itafuzu Fainali zijazo za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Juni mwaka huu nchini Misri, kila mchezaji atapatiwa bakhshishi ya Sh. Milioni 10.
Katika ziara yake hiyo, Waziri Mkuu Majaliwa aliwaambia wachezaji kwamba Serikali na wananchi wana matumaini makubwa kwa timu yao, hivyo wahakikishe wanapata ushindi katika mechi yao dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda na wasiwe na wasiwasi kwa sababu hawana tofauti yoyote na wachezaji wa timu nyingine duniani.
“Macho yote ya Watanzania yameelekezwa katika mechi ya kesho na Serikali ina matumaini makubwa na timu ya Taifa, hivyo waelewe kwamba kesho ni siku muhimu sana. Lengo letu ni kufikia hatua ambayo mataifa mengine yamefikia”alisema.
Awali ya hapo, Mwenyekiti wa Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema kwamba kamati yake itatoa Sh. Milioni 10 kwa kila mchezaji wa timu hiyo itaifunga Uganda kesho katika mchezo wa mwisho wa Kundi L na kufuzu AFCON ijayo nchini Misri.
Makonda amesema Watanzania wanachokijua kwa sasa ni kwamba AFCON 2019 ni zamu yao, hivyo amewaomba wachezaji wa timu ya Taifa wahakikishe wanawapa furaha kwa kuifunga timu ya Taifa ya Uganda na kwamba wananchi wengi wamehamasika kwenda kuwashangilia.
Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangala aliahidi kuwapeleka katika mbuga ya wanyama kwa ajili ya mapumziko iwapo wachezaji hao wataibuka na ushindi katika mechi yao dhidi ya Uganda kesho.
Dk. Kigwangala alisema Serikali ipo pamoja na wanamichezo, ambapo amewataka wachezaji hao wa timu ya Taifa wakapigane kweli kweli kwa ajili ya Taifa lao. “Kesho muingie uwanjani kama askari wa nchi. Mkapiganie ushindi wa Taifa letu”.
Awali, Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samata alisema; “Ninafuraha si kwa sababu ya ukubwa wa mechi ya kesho bali ni kwa sababu naona kesho nakwenda kuongoza nchi. Tupo tayari kuliletea Taifa ushindi,”.
Machi 24, 2018; Taifa Stars ilishinda 3-0 dhidi ya Uganda katika mchezo wa mwisho wa kufuzu AFCON 2019 Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam, mabao ya Simon Msuva dakika ya 21, Erasto Nyoni kwa penalti dakika ya 51 na Aggrey Morris dakika ya 57.
Kwa ushindi huo, Taifa Stars imetimiza ndoto za kufuzu AFCON kama mshindi wa pili wa kundi L ikifikisha pointi nane, nyuma ya Uganda iliyomaliza na pointi 13 wakizipiku Lesotho iliyomaliza na pointi sita na Cape Verde pointi tano.    
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Aishi Manula, Hassan Kessy, Gardiel Michael, Kelvin Yondan, Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Simon Msuva/Thomas Ulimwengu dk89, Mudathir Yahya, John Bocco/Feisal Salum dk81, Mbwana Samatta na Farid Mussa/Himid mao dk70.
KIKOSI KILICHOITWA; Makipa; Aishi Manula (Simba SC), Aaron Kalambo (Tanzania Prisons), Metacha Mnata (Mbao FC) na Suleiman Salula (Malindi SC).
Mabeki; Hassan Kessy (Nkana FC - Zambia), Gardiel Michael (Yanga SC), Kelvin Yondan (Yanga SC), Vincent Philipo (Mbao FC), Ally Mtoni ‘Sonso’ (Lipuli FC), Andrew Vincent ‘Dante’ (Yanga SC), Kennedy Wilson (Singida United) na Aggrey Morris (Azam FC).
Viungo;  Feisal Salum (Yanga SC), Jonas Mkude (Simba SC), Himid Mao (Petrojet FC - Misri), Mudathir Yahya (Azam FC), Shiza Kichuya (ENPPI - Misri), Simon Msuva (Difaa El Jadida – Morocco) na Farid Mussa (Tenerife B).
Washambuliaji; Yahya Zayd (Ismailia - Misri), Shaaban Iddi Chilunda (CD Izara – Hispania), Rashid Mandawa (BDF XI - Botswana), Thomas Ulimwengu (JS Saoura - Algeria), John Bocco (Simba SC) na Mbwana Samatta (KRC Genk – Ubelgiji).
Machi 25, 2019; Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Joseph Magufuli aliagiza wachezaji wote wa Taifa Stars iliyofanikiwa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) Juni mwaka nchini Misri wapatiwe viwanja katika eneo zuri mjini Dodoma.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo Ikulu mjini Dar es Salaam siku hiyo alipokutana na wachezaji wa Taifa Stars kuwapongeza kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Uganda Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam hivyo kuiwezesha nchi kufuzu AFCON kwa mara ya pili tu kihistoria baada ya mwaka 1980 nchini Nigeria.
Pamoja na wachezaji, ofa ya viwanja wamepewa pia wachezaji wawili waliokuwemo kwenye kikosi cha Taifa Stars iliyofuzu AFCON ya mwaka 1980, beki Leodegar Tenga na mshambuliaji, Augustino Peter, maarufu kama Peter Tino.
Ofa ya kiwanja amepewa pia bondia Hassan Mwakinyo aliyealikwa pia Ikulu leo baada ya kumshinda kwa Knockout (KO) raundi ya tano Muargentina, Sergio Eduardo Gonzalez juzi mjini Nairobi nchini Kenya.
Kwa Peter Tino, pamoja na kiwanja Rais Magufuli alimzawadia fedha taslimu Sh. Milioni 5 kama mtaji wa kwenda kufanya biashara ya kuendesha maisha yake. 
Kwa wachezaji, mbali ya zawadi ya viwanja ya Rais, kila mmoja atapatiwa donge nono la Sh. Milioni 10, ahadi ya Kamati ya Saidia Taifa Stars Ishinde, chini ya Mwenyekiti, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.  
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano, Kassim Majaliwa ameshauri ya Saidia Taifa Stars Ishinde, chini ya Mwenyekiti wake, Makonda iendelee na jukumu hilo na kwamba ihusishwe pia kwenye kampeni za timu nyingine za taifa na hata klabu ikibidi.  
Mei 1, mwaka 2019 Kocha Amunike alitaja kikosi cha awali cha wachezaji 39 kwa ajili ya Fainali za AFCON na mchezo wa kirafiki dhidi ya Misri Juni 13, mwaka huu Uwanja wa Borg El Arab mjini Alexandria.
Makipa; Aishi Manula (Simba SC), Metacha Mnata (Mbao FC), Suleiman Salula (Malindi SC) na Aaron Lulambo (Tanzania Prisons).
Mabeki; Claryo Boniface (U20), Hassan Kessu (Nkana FC, Zambia), Vincent Philipo (Mbao FC), Shomari Kapombe, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Erasto Nyoni (Simba SC), Kelvin Yondan, Gardiel Michael (Yanga SC), Abdi Banda (Baroka FC, Afrika Kusini), Ally Mtoni (Lipuli FC), David Mwantika, Aggrey Morris (Azam FC), Ally Ally (KMC) na Kennedy Wilson (Singida United).
Viungo; Feisal Salum, Ibrahim Ajibu (Yanga SC), Himid Mao (Petrojet, Misri), Frank Domayo, Mudathir Yahya (Azam FC), Jonas Mkude (Simba SC), Shiza Kichuya (ENNPI, Misri), Simon Msuva (Difaa Hassan El-Jadidi Morocco), Farid Mussa (Tenerife, Hispania) na Freddy Tangalu (Lipuli FC).
Washambuliaji; Yahya Zayd (Ismailia, Misri), Shaaban Iddi Chilunda (Tenerife, Hispania), Rashid Mandawa (BDF, Botswana), Ayoub Lyanga (Coastal Union), Kassim Khamis (Kagera Sugar), Miraj Athumani (Lipuli FC), Kelvin John (Serengeti Boys), Adi Yussuf (Solihull Moors, England), John Bocco (Simba SC), Thomas Ulimwengu (JS Saoura, ALgeria) na Nahodha Mbwana Samatta (KRC Genk, Ubelgiji).  
Juni 1, 2019 mshambuliaji mpya wa Blackpool FC ya Daraja la Pili England, Adi Yussuf alikuwa miongoni mwa wachezaji walioripoti katika kambi ya Taifa Stars hoteli ya White Sands mjini Dar es Salaam katika siku ya kwanza kwa maandalizi ya AFCON.
Juni 6, 2019; Kocha Amunike aliwaengua wachezaji saba kwa sababu mbalimbali, mabeki Kennedy Wilson wa Singida United, Ally Ally wa KMC, Shomari Kapombe, viungo Jonas Mkude (wote wa Simba), Ibrahimu Ajibu wa Yanga na washambuliaji Khamis Khamis wa Kagera Sugar na Ayoub Lyanga wa Coastal Unon ya Tanga.
Wengine wote hawakukidhi mahitaji ya falsafa zake, lakini Kapombe pekee inafahamika ni majeruhi.
Juni 7, 2019; Kikosi cha Taifa Stars kiliondoka na wachezaji 32 kwenda kambini mjini Alexandria, Misri baada ya kuchujwa saba na kati ya hao ni 23 tu watashiriki AFCON.
, wakati wengine wataendelea kubaki kambini kwa maandalizi ya michuano ya Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN), inayohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.
Naam, hiyo ndiyo safari ya Taifa Stars Misri 2019.
Share on Google Plus

About Mahmoud Bin Zubeiry

Mahmoud Zubeiry Works at BIN ZUBEIRY "BIN ZUBEIRY" Tangaza nasi hapa.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment