Monday, October 23, 2023

HAFLA YA UTAMBULISHO WA MRADI WA UJENZI WA BARABARA YA KM 10.7 KWA KIWANGO CHA LAMI MANISPAA YA TABORA

Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa ushirikiano na Wakala wa ujenzi wa Barabara za Mjini na Vijijini ( TARURA) Wilaya ya Tabora, imetambulisha mradi wa ujenzi wa Barabara yenye umbali wa kilometa 10.7 za kiwango cha lami katika Manispaa yake, mradi ambao unafadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Mkopo wa Benki ya Dunia kupitia Mradi wa Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji ya Tanzania kwa Kuhusisha Ushindani ( TACTIC).

Manispaa ya Tabora imetangaza mradi huu leo Oktoba 23,2023 katika ukumbi wake, kupitia kwa Madiwani wake hususani madiwani ambao mradi unapita kwenye Kata zao, Madiwani ambao ni wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Mipangomiji, Wakuu wa Taasisi mbalimbali ambao ni wadau wakubwa katika mradi huu kama TANROADS Mkoa wa Tabora, Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Manispaa ya Tabora (TUWASA), TTCL, TANESCO Pamoja na Wakuu wa Sehemu na Vitengo wa Halmashauri.

Katika utambulisho huo, Kampuni ya Chongqing International Construction Corporation (CICO) ndio kampuni ambayo imeshinda zabuni ya kujenga Barabara hizi zenye urefu wa kilometa 10.7 kwa thamani ya fedha za kitanzania bilioni 16.689 kwa muda wa miezi 15 tokea kukabidhiwa eneo la kazi.

Barabara zitakazojengwa kwa awamu hii ya mradi ni Pamoja na Barabara ya SWETU yenye Km 3.9, Barabara ya KISARIKA i ,ii, iii , yenye Km 2.99, Barabara ya KANYENYE i , ii, iii , yenye Km 1.09 pamoja na Barabara ya MAILTANO i , ii, iii yenye Km 2.418.

Aidha UNITEC Civil Consultants Ltd, ndio Mhandisi mshauri wa miradi yote itakayojengwa katika Manispaa ya Tabora kwa awamu zote za mradi wa TACTIC katika Manispaa ya Tabora.

Madiwani wenyeji wa mradi unakopita, Madiwani wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Mipangomiji Pamoja na Wajumbe wote waliokuwepo wameupokea mradi kwa mikono miwili na kuishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuithamini na kuipa kipaumbele Manispaa ya Tabora kwa mradi huo ambao unaenda kupunguza adha ya Barabara mbovu mjini hapa.

Sambamba na hilo, madiwani pia wamependekeza kuwa ,sehemu zenye uwezekano, vibarua katika ujenzi wa mradi huu wapewe kipaumbele vijana wakazi wa Kata husika mradi ulipo ili vijana hao nao wapate ajira zitokanazo na mradi huu.

Mwenyeketi katika hafla hii ya mapokezi ya mradi Mhe. Kessy Abdurahman, ambae ni Diwani wa Kata ya Gongoni, akimwakilisha Meya wa Manispaa ya Tabora Mhe. Ramadhan Kapela, amezitaka taasisi zote ambazo ni wadau wakubwa wa kutoa huduma za kijamii kama TANESCO, TUWASA, Pamoja na TTCL kumpa ushirikiano mkubwa mkandarasi huyu ili aweze kumaliza kazi kwa wakati kwani muda mwingine watatakiwa kuhamisha miundombinu ya huduma wanazozitoa kupisha ujenzi wa Barabara lakini pia akasisitiza Mkandarasi azingatie ubora uliokusudiwa katika ujenzi wa mradi huu.



No comments:

Post a Comment