Katibu mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Komredi Daniel Godfrey Chongolo ameonekana kutoridhishwa na hatua ya Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya katika Halmashauri ya Sumbawanga Vijijini, ambapo ameagiza Serikali mkoani Rukwa pamoja na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kutuma timu ya uchunguzi ili kubaini kinachokwamisha mradi huo kukamilika, huku ukionekana kutekelezwa chini ya kiwango cha ubora na thamani ya fedha kilichopelekewa hadi sasa.
Mbali na kutoridhishwa na ujenzi huo wa hospitali unavyotekelezwa, Komredi Chongolo pia alionekana kukerwa na mkandarasi wa Mradi wa Maji wa Ilemba, Jimbo la Kwela, ambaye pamoja na RUWASA Mkoa wa Rukwa kumwekea msukumo ili ajenge kwa kasi ya kukamilisha ndani ya muda wa mkataba, bado ameendelea kusuasua huku akitoa visingizio vingi vya kutomaliza kazi hiyo kwa wakati ili wananchi wa Kata ya Ilemba, Vijiji vya Ilemba A na B na Kata ya Kaswepa, wapate maji safi na salama ya kutumia.
“Mkuu wa Wilaya, hakuna kucheka na waliopewa kazi hizi. Tukiacha hali hii, mambo hayataenda na hiyo sio sawa hata kidogo. Hatuwezi kuacha mambo yaende namna hii. Tutakuwa hatutendi haki na tutakuwa hatujitendei haki wenyewe na nafasi zetu za kuwatumikia wananchi. Wananchi wanachotaka ni huduma. Huko aliko anakosema anauguliwa, kuna Mkuu wa Wilaya mwenzako, wasiliana nae upate uhakika na akija aje na Ushahidi wa kuwa alikuwa anauguliwa.
“Vinginevyo ikifika tarehe 30 mwezi huu ambao mkataba wake ulikuwa unakamilika, asiongezewe mkataba. Tusitengeneze mazingira ya watu kucheza na miradi ya maendeleo na fedha za umma kama zao binafsi. Wekeni utaratibu, mwezi mmoja hajamaliza kazi mnavunja mkataba na mtengeneze mbadala kwa kutumia Force Account. Tunataka watu wapate maji, sio vinginevyo,” amesema Chongolo.
Komredi Chongolo ametoa maelekezo hayo Oktoba 10, 2023 akiwa katika Kata ya Mtowisa na Ilemba, mara baada ya kukagua mradi huo wa Maji wa Ilembo wa Tsh. 1.9 bilioni ambao bado uko asilimia 27 na hospitali ya wilaya iliyoanza kujengwa tangu Disemba 2021 na mkandarasi aitwae Kuyella Enterprises, huku ukitakiwa kukamilika Machi 2022, lakini hadi alipofika mahali hapo kuutembelea na kuukagua, ulikuwa haujakamilika.
Katika hatua nyingine msafara wa Katibu Mkuu huyo wa Chama cha Mapinduzi, umesimamishwa maeneo ya Mwela, Mtowisa, Msia, Talanda, Milepa na Kinambo, Milepa akelekea Kioze na Ilemba, ambapo wananchi walitaka awasikilize changamoto zao na kuzitolea maelekezo ya kuzitafutia ufumbuzi.
Katika eneo la Kijiji cha Mwela, Kata ya Mtowisa, watu mbalimbali wakiwemo akina mama na vijana kijiji hicho, kilichopo Halmashauri ya Sumbawanga Vijijini walisimamisha msafara wakiwa na ndoo za maji, wakitaka awaondolee kero ya uhaba wa maji na namba ya utambulisho wa kijiji hicho.
"Huduma za afya tunazo...umeme tunao...barabara inapitika...hata pembejeo za kilimo tunapata. Hatuna tatizo na huduma zingine Katibu Mkuu wa CCM. Changamoto zetu hapa ni mbili tu, maji haya unavyoyaona si salama wala si safi. Lakini pia tuna changamoto ya namba ya kijiji chetu hiki kutotambuliwa huko wilayani," alisema mwananchi aliyejitambulisha kuwa ni Mwenyekiti wa Wananchi hao.
Kufuatia hali hiyo Komredi Chongolo aliwatuliza wananchi hao kwa kutoa maelekezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Mhe. Nyakia Ally kuhakikisha changamoto za wanakijiji hao zinatatuliwa ndani ya muda mfupi, ikiwa ni pamoja na kukutana nao kwenye kikao akiwa na timu yake ya wataalam kutoka wilayani, siku ya Ijumaa, wiki hii ili wajadiliane nao namna ya kutatua kero hizo kwa njia shirikishi. Ndugu Chongolo aliahidi kufuatilia suala hilo kwa ukaribu.
Ndugu Chongolo alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, kwa kutumia RUWASA, wapeleke gari la kuchimba kisiama katika kijiji hicho kwa haraka, wakati wakiendelea kutafuta vyanzo vingine vya uhakika, baada ya Meneja wa RUWASA kutoa taarifa kuwa katika mipango yao kijiji hicho kiko ndani ya maeneo ambayo yamepangiwa mradi wa maji utakaogharimu Tsh. 1.3, utakaokuwa mwarobaini wa kero hiyo.
Mbali ya kutembelea miradi hiyo ya Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya, mradi wa Maji Ilemba na kuzungumza na wananchi katika maeneo hayo, pamoja na kwingine alikosimamishwa, Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Chongolo pia alitembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Kaoze na kuzungumza na wananchi wa kata hiyo, kabla ya hitimisha ziara yake Jimbo la Kwela, kwa kuzungumza na wananchi wa Kata ya Kilyematundu, Sumbawanga Vijijini.
No comments:
Post a Comment