DORIS MOLLEL WAIPONGEZA SERIKALI KUKUBALI KUONGEZA LIKIZO KWA WANAOJIFUNGUA WATOTO NJITI

NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

TAASISI ya Doris Mollel imeipongeza Serikali kwa kukubali ombi la kuongeza siku za likizo kwa wanawake wanaojifungua watoto njiti nchini ili kulinda afya ya mama na mtoto ambapo huamuzi huo ulitangazwa na Makamu wa Rais Dkt. Philipo Mpango katika sherehe za Mei Mosi Jijini Arusha.

Akizungumza na Waandishi wa habari leo Mei 3, 2024 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Doris Mollel, Bi. Doris Mollel amesema Serikali ilibainisha kwamba kuanzia sasa iwapo mfanyakazi atajifungua mtoto njiti, kipindi cha uangalizi maalum hakitahesabika kama likizo ya uzazi.

“Likizo ya uzazi itaanza tu baada ya kumalizika kwa kipindi hicho cha uangalizi, kadiri madaktari watakavyothibitisha. Vilevile, mfanyakazi husika ataruhusiwa kutoka kazini saa 7:30 mchana kila siku kwa muda wa miezi sita baada ya kumalizika kwa likizo ya uzazi, ili kumpa fursa ya kwenda kunyonyesha”. Amesema Bi. Mollel

Aidha amesema Taasisi hiyo inatambua mchango wa wadau mbalimbali walioshirikiana na Taasisi katika kuanzisha Mchakato wa kuiomba Serikali kufanya marekebisho kwenye sheria ya likizo ya uzazi ambao ulianza mwaka 2017, ambao ni pamoja na Wataalam wa Afya, Wazazi wa watoto njiti, Wataalam wa Sheria, Chama cha Madaktari wa Watoto Wachanga, Umoja wa Wake wa Viongozi, Mtandao wa Haki ya Afya ya Uzazi, Shirika la Kazi Duniani (ILO), na Wadau wa Utatu ambao ni Chama cha Waajiri (ATE), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), na Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE).

Amesema Taasisi ya Doris Mollel inatambua kwa dhati mchango usiopimika wa wadau wa maendeleo, hasa Women Fund Tanzania Trust, Asas Group, na Segal Family Foundation.

“Vilevile, tunatoa shukrani zetu za dhati kwa waandishi vinara wa watoto njiti, ambao wamesaidia kusambaza na kupigania ajenda mbalimbali zinazohusu watoto njiti”. Ameeleza

Pamoja na hayo amesema , Taasisi ya Doris Mollel iko tayari katika kushiriki kwa kina katika hatua zote zinazofuata za kuendeleza na kuhakikisha uamuzi huo unajumuishwa katika Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, kwa ushirikiano thabiti na wadau weo, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE).

Kwa Upande wake Dkt.Dinnah Richard kutoka Taasisi ya Women Fund (WF) amesema  wanatamani kuona mambo yaliyoongelewa na Serikali katika siku ya wafanyakazi kuhusiana na kuongezwa kwa likizo ya wanawake wafanyakazi wanapojifungua watoto njiti yanaingizwa kwenye Sheria ili kuwepo kwa utekelezaji suala hilo.

"Tunatamani sana yale yaliyoongelewa yaingie kwenye sheria maana bila Sheria hatutajua yanatekelezwa au hayatekelezwi,kwa Umoja wetu na sauti zetu  tunafanya kazi na serikali ili sheria  hiyo iweze kufanya kazi"Bi.Dinnah amesema.

Share on Google Plus

About emmanuel mbatilo

Mahmoud Zubeiry Works at BIN ZUBEIRY "BIN ZUBEIRY" Tangaza nasi hapa.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment