ZAIDI ya wakazi 3000 waishio kwenye vijiji vya karibu na hifadhi ya Taifa ya Serengeti wanatarajiwa kupatiwa elimu ya namna ya kukabiliana na changamoto za Wanyama hususani Simba.
Elimu ya kukabiliana na Simba pamoja na wanyama wengine wakali, inatolewa kupitia Filamu inayojulikana kama 'Kuishi na Simba' iliyotengenezwa na Msanii qa Filamu nchini, Erica Rugabandana.
Filamu hiyo inalenga kufahamu hatari za kukabiliana na wanyama wakali ambao hutoka hifadhini na kwenda kwenye makazi ya watu akimuangazia zaidi Simba.
Pia, inasaidia kufahamu uhusiano wa Simba hao na binadamu, namna wanavyosambaa kwenye jamii na tabia zao.
Mbali na hilo, filamu hiyo inatoa elimu ya namna ya kulisha mifugo kwa wananchi wanaoishi karibu na hifadhi wanakohifadhiwa Simba hao ili kuepuka hatari ya kushambuliwa.
Tafiti zinaonyesha kuwa katika asilimia 40 ya Simba pori waliosalia duniani, Tanzania ni kinara katika uhifadhi wa Simba hao.
Kwa mujibu wa Erica, filamu hiyo ni muhimu kwa jamii zinazoishi na Wanyamapori si kwa Tanzania pekee bali Afrika Mashariki ikiwamo Kenya, Uganda, ambako kumekuwa na visa vingi vya Simba kushambulia mifugo na binadamu.
"Ninaamini kwamba filamu hii itasaidia hata kuleta mijadala ya migogoro ambayo imekuwa ikitokea baina ya Binadamu na Wanyamapori na hivyo mamlaka husika nchini Tanzania kuweka mikakati juu ya uhifadhi bora wa Wanyamapori hao na ambazo zitasaidia kutoa taarifa za utungaji sera, programu za elimu na ushirikishwaji wa jamii katika masuala haya,"alisema Erica.
Alisema tayari filamu hiyo imeanza kuonyeshwa kwenye shule na maeneo ya jamii zinazoishi karibu na mbuga za kitaifa Kaskazini mwa Tanzania.
"Filamu hii imeonyeshwa kote ulimwenguni ikiwa no pamoja na Tamasha la Filamu la Australia la Wild Earth Oceania maperma mwaka huu na itaonyeshwa katika Ubalozi wa Australia nchini Kenya mwezi ujao kama sehemu ya tamasha pekee la filamu za wanyamapori barani Afrika, Pridelands Wildlife Film Festival,"alisema Erica.
0 comments:
Post a Comment