Na Jovina Bujulu, Maelezo Dodoma.
Muungano wa Tanzania kwa miaka 50 umekuwa ni undugu hivyo kuufuta ni sawa na kufuta utaifa wetu na kukaribisha ukabila.
Hayo yamesemwa leo mjini Dodoma, na Kapteni John Chiligati ambaye ni mjumbe aw Bunge Maalum la Katiba wakati wa mahojiano na kipindi cha Jambo kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha TBC One.
Aliendelea kusema kwamba muundo wa kimaisha wa Muungano wetu ni wa serikali mbili, hivyo tusivunje kabisa Muungano huo.
"Kuvunja Muungano ni kukaribisha ukabila na kuchanganya wananchi maana watajitenga kwamba wengine ni Wazanzibar, wengine ni Watanganyika, hivyo ni kurudi nyuma badala ya kusonga mbele" aliongeza Mhesh Chiligati.
Akizungumzia madhara ya serikali tatu Mhesh Chiligati alisema kwamba Serikali tatu italeta utata maana kutakuwa na Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Muungano. Kwa muundo huo Serikali tatu, serikali ya Muungano haitakuwa na watu, madaraka,utaifa na hata pesa zake.
Akichangia ya kuwa na serikali mbili, Mzee maarufu Mjini Dodoma Jumanne Gombashi alisema kwamba suala la zaidi ya Serikali mbili si tatizo la Watanzania, hivyo tusiwasingizie kwamba wanahitaji serikali tatu , kwani badala ya kutatua matatizo tutaongeza matatizona tutakuwa tunaicha chana nchi yetu.
" Tumekuwa na Serikali mbili kwa miaka 50, kama kuna makosa hatuna budi kujitathmini, na kujisahihisha na kujikosoa ili tutatue matatizo hayo na tuendelee na Serikali mbili.." alisema mzee Gombashi.
Aidha aliendelea kusema kwamba tunapozungumzia serikali tatu tuangalie pia upande wa gharama za uendeshaji wa Serikali hizi. Kila upande yaani Zanzibar na Tanzania Bara utatakiwa kuchangangia uendeshaji wa serikali ya Muungano, na pia tutalazimika kuwa na viongozi watatu, mabaraza ya mawaziri matatu na mabunge matatu.
"Kwa kuwa na serikali tatu hawa watu wote wanahitaji huduma kwa hiyo kwa kufanya hivyo tutapanua matumizi kwa nchi changa kiuchumi kama hii yetu" alisema mzee Gombashi.
Mhesh. Chiligati alitoa ushauri wa kudumisha Muungano,na kuepuka muundo utakaodhoofisha Muungano bali tuhakikishe Muungano unaimarishwa na pande sote mbili.
Naye mzee Gombashi alimalizia kwa kuwahimiza Watanzania kutotetereka na kuburuzwa na watu wasiopenda Muungano, na kwamba iko siku tutafika kwenye serikali moja na tuwe wamoja zaidi
0 comments:
Post a Comment