Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo amesema amefarijika kuona wanufaika wa Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi wanafanyia kazi Mafunzo hayo kwa kuzalisha bidhaa mbalimbali kupitia Ujuzi waliojifunza.
Prof. Nombo amesema hayo leo Octoba 13, Kibaha, Pwani alipotembelea banda la Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) katika maonesho ya Maadhimisho ya Juma la Elimu ya Wazima yaliyoanza tangu Octoba 9 na leo ikiwa ndiyo kilele cha maadhimisho hayo.
Akiwa katika banda la TEA, Prof. Nombo alikutana na baadhi ya wanufaika wa Mafunzo ya Kuendeleza Ujuzi yaliyotolewa kupitia ruzuku ya Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF), ruzuki hiyo ikiwa ni fedha kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na ufadhili wa Benki ya Dunia ambayo hadi mafunzo yanakamilika zaidi ya Watanzania 49,000 walinufaika na mafunzo hayo.
Prof. Nombo amesema, ni jambo la kufurahisha kuwaona wanufaika hao wamethubutu kufanyia kazi kile walichojifunza na kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwa na ubunifu mkubwa ndani yake hivyo, ni wakati muafaka sasa waanze kuzitangaza bidhaa hizo ili kujiongezea wigo mpana wa soko.
‘‘Hizi bidhaa mnazozalisha ni nzuri na nina uhakika zina soko kubwa tuu hapa nchini, anadaeni mikakati ya kuzitangaza ili ziwafikie Watanzania wengi zaidi na mwisho wa siku soko lake lizidi kukua ili muweze kufikia malengo yenu hasa katika ujasiriamali, amesema Prof. Nombo’’
Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), imeshiriki maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima kupitia Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi ambao unatoa Mafunzo ya Ujuzi kwa lengo la kuwasaidia Watanzania kujihusisha kwenye shughuli za uzalishaji mali ili kujikwamua kiuchumi.
0 comments:
Post a Comment