FURSA YA UFADHILI WA MASOMO CHUO KIKUU HURIA CHA TANZANIA


SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatekeleza Mradi wa miaka mitano wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), ambao umefadhiliwa na Benki ya Dunia na unatekelezwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania huku ukisimamiwa vyema na Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.

Kupitia Mradi huu wa HEET, Serikali inatoa ufadhili kwa watoto wa kike kwenye masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati, wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini na zinazotambuliwa na TASAF, RITA n.k, walemavu, yatima au kutoka katika maeneo ambayo kijiografia hayajafaidika.

Ufadhili utazingatia maeneo yafuatayo, ada ya masomo, gharama za chakula na malazi, vifaa vya kujifunzia, shajara, bima ya afya, Kishikwambi, nauli ya kutoka nyumbani kwenda kituo cha mafunzo na kurudi nyumbani baada ya kuhitimu.

Wanafunzi watakaohitimu na kufaulu masomo katika programu hii watapata fursa ya kuomba udahili katika Taasisi za Elimu ya juu nchini kwa kufuata taratibu zilizoainishwa na TCU, NACTIVET na chuo husika, ikiwa ni pamoja na sifa za kuomba mkopo wa masomo ya elimu ya juu kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Tanzania bara na Tanzania visiwani.

Sifa za kujiunga na ufadhili huu: Uwe na Cheti cha Sekondari (Kidato cha nne) kikiwa na ufaulu wa angalau masomo manne kikijumuisha na cheti cha kidato cha sita chenye angalau alama 1.5 katika masomo mawili kwenye tahsusi za masomo ya sayansi (Fizikia, Kemia, Baolojia, Hisabati, Uchumi na Jiografia).

AU

Diploma katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati kutoka kwenye chuo kinachotambulika na serikali yenye ufaulu wa GPA ya 2.0 mpaka 2.9.

NB: Programu hii itafundishwa kwa njia ya ana kwa ana na mihadhara ya mtandaoni (Blended mode).

Kuweza kutuma maombi ya ufadhili huu, jaza fomu ya maombi ambayo inapatikana kwenye vituo vyote vya mikoa vya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Bara na Visiwani (Unguja na Pemba).

Aidha fomu inapatikana katika tovuti ya chuo (www.out.ac.tz). Fomu ikishajazwa irudishwe kwenye kituo cha mkoa husika. Au unaweza kutuma fomu iliyojazwa vyema kupitia baruapepe ya (ofpheet@out.ac.tz)

Hakuna gharama za maombi katika kuomba ufadhili huu na mwisho wa kupokea maombi itakuwa Agosti 30, 2024.
Share on Google Plus

About emmanuel mbatilo

Mahmoud Zubeiry Works at BIN ZUBEIRY "BIN ZUBEIRY" Tangaza nasi hapa.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment