KAMATI YA BARAZA LA WAWAKILISHI ZANZIBAR YAJA BARA KUJIFUNZA USALAMA NA AFYA KAZINI

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mtumwa Peya Yusuph na Katibu wa Kamati hiyo, Ndg. Abubakar Mahmoud Iddi, wakifuatilia wasilisho la Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam.


**************************

Na Mwandishi Wetu

Kamati ya Kudumu ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar imetembelea Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na baadhi ya viwanda vinavyosimamiwa na OSHA lengo likiwa ni kujifunza mfumo wa usimamizi wa masuala ya usalama na afya kwa upande wa Tanzania Bara ili kushauri maboresho stahiki kwa upande wa Zanzibar.

Ziara hiyo imejumuisha wajumbe wa Kamati tajwa pamoja na watumishi wa Idara ya Usalama na Afya Kazini iliyopo ndani ya Ofisi ya Rais-Kazi, Uchumi na Uwekezaji-Zanzibar.

Ujumbe huo umefika Ofisi za OSHA Dar es Salaam na kupata wasilisho kuhusu utendaji wa Taasisi toka kwa Mtendaji Mkuu, Bi. Khadija Mwenda, ikiwemo hatua ambazo Taasisi hiyo imepitia kutoka kuwa Idara ya Ukaguzi wa Viwanda katika Wizara yenye dhamana ya Masuala ya Kazi hadi kuwa Taasisi inayojitegemea.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mtumwa Peya Yusuph, amesema wanatambua kwamba OSHA Tanzania Bara ipo mbali katika usimamizi wa masuala husika jambo ambalo limewasukuma kuja kujifunza ili kuishauri Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuboresha mfumo wa usimamizi wa masuala ya usalama na afya kwa upande wa Zanzibar.

“Tunatambua kwamba wenzetu huku bara mnafanya vizuri sana katika usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi hivyo tumeona ni busara kuja kujifunza ili tuweze kuchukua mazuri yaliyopo na tuishauri Serikali yetu kuyafanyia kazi,” ameeleza Mwenyekiti huyo wa Kamati na kuongeza:

“Tunawapongeza sana OSHA kwa kazi kubwa wanayofanya katika kuboresha usalama na afya kwenye maeneo ya kazi nchini kama tulivyoona katika wasilisho la Mtendaji Mkuu pamoja na hali halisi ya utekelezaji wa miongozo ya OSHA kwenye viwanda tulivyotembelea ambapo tumeona wahusika wamejitahidi kuzingatia taratibu muhimu za usalama na afya kwa ajili ya kuwalinda wafanyakazi.”

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, amesema ziara hiyo ni muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya biashara na uwekezaji kote Tanzania Bara na Zanzibar kutokana na uhalisia kwamba wawekezaji wengi wamewekeza bara na visiwani na hivyo ni muhimu kuwa na mifumo na sheria zinazoendana.

“Tumeshasaini hati ya mashirikiano na wenzetu wa Idara ya Usalama na Afya Kazini Zanzibar hivyo tupo tayari kushirikiana nao katika kufanya maboresho wanayokusudia ili kama nchi tuwe na mifumo na viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa,” ameeleza Bi. Mwenda.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Usalama na Afya Kazini Zanzibar, Bw. Ame Faki Saleh, amesema wanayo matumaini kuwa kupitia mashirikiano na OSHA Bara ambayo imeshapiga hatua kubwa katika usimamizi wa usalama na afya watajifunza mambo mengi yatakayosaidia kufanikisha safari ya mabadiliko ya Idara yao kuwa Taasisi inayojitegemea kwa upande wa Zanzibar.

Mkurugenzi wa Mahusiano wa Makampuni ya Bakhresa, ambako ni miongoni mwa maeneo yaliyotembelewa na Kamati, Bw. Hussein Sufiani ametoa ushuhuda kwamba makampuni ya Bakhresa yamepata mafanikio makubwa katika biashara ndani na nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na kutekeleza ipasavyo sheria za nchi ikiwemo miongozo ya OSHA kuhusu usalama na afya kazini.

Ziara hiyo ya Kamati inafanyika kwa siku mbili katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma ambapo maeneo yaliyotembelewa ni pamoja na Kiwanda cha Berger Paints International Ltd na Kiwanda cha Unga cha Bakhresa (Dar es Salaam) pamoja na Kiwanda cha Mbolea cha Intracom na Mji wa Serikali Mtumba (Dodoma).

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na watumishi wa Idara ya Usalama na Afya Kazini Zanzibar, wakifuatilia wasilisho la Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, wakati wa ziara ya Kamati hiyo katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam. Lengo la ziara hiyo ilikuwa ni kujifunza jinsi Taasisi hiyo ilivyoweza kuku ana kufikia kuwa Taasisi inayojitegemea kutoka kuwa Idara katika Wizara.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda, akifanya wasilisho kuhusu hatua mbalimbali ambazo OSHA imepitia katika ukuaji wake wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar pamoja na watumishi wa Idara ya Usalama na Afya Kazini Zanzibar katika Ofisi za OSHA Jijini Dar es Salaam.

Ujumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, watumishi wa Idara ya Usalama na Afya Kazini Zanzibar wakiwa wameambatana na wenyeji wao OSHA Tanzania Bara wakitazama uzingatiaji wa taratibu muhimu za usalama na afya katika shughuli za uzalishaji za Kiwanda cha Berger Paints International Ltd.

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Bi. Khadija Mwenda (kushoto) akifafanua jambo katika kikao cha awali katika kiwanda cha Bakharesa Food Products Ltd kilichopo Buguruni Dar es Salaam wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika kiwanda hicho.

Mkurugenzi wa Mahusiano wa Makampuni ya Bakhresa, Bw. Hussein Sufiani (mwenye Kaunda suti nyeusi), akiuongoza ujumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ulioambatana na Idara ya Usalama na Afya Kazini na Menejimenti ya OSHA katika ziara ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya kazini kwa Tanzania Bara katika Kiwanda cha Bakhresa Food Products Ltd kinachozalisha unga wa ngano kilichopo Buguruni, Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe. Mtumwa Peya Yusuph, akitoa neno la shukrani kwa Menejimenti ya OSHA mara baada ya kuhitimisha ziara ya kujifunza kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Usalama na Afya kazini kwa upande wa Tanzania Bara.

Mkurugenzi wa Mahusiano wa Makampuni ya Bakhresa, Bw. Hussein Sufiani (mwenye kaunda suti nyeusi), akieleza jinsi Kiwanda cha Bakhresa Food Products Ltd cha Buguruni kinavyotekeleza Sheria ya Usalama na Afya kazini katika shughuli zake mbele ya ujumbe wa Kamati ya Kudumu ya Utalii, Biashara na Kilimo ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar ulioambatana na Idara ya Usalama na Afya Kazini ya Zanzibar na Menejimenti ya OSHA katika ziara ya mafunzo.


Share on Google Plus

About emmanuel mbatilo

Mahmoud Zubeiry Works at BIN ZUBEIRY "BIN ZUBEIRY" Tangaza nasi hapa.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment