Mama Lishe Mkoa wa Dar es Salaam Wapokea Mitungi 1,000 ya Gesi ya Kupikia kutoka Puma Energy

 KAMPUNI ya Puma Energy Tanzania imetoa mitungi 1,000 ya gesi ya kupikia kwa Mama Lishe wa Mkoa wa Dar es Salaam ili kuhakikisha kampeni ya nishati safi inafanikiwa kwani dhamira ya Rais ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano hayo yaliyofanyika leo Oktoba 11, 2024 katika viwanja Vya Biafra, Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa huo, Albert Chalamila amesema kuwa Mkoa wa Dar es Salaam ni kinara wa matumizi ya nishati chafu, hivyo uwamuzi wa Kampuni ya Puma Energy Tanzania kugawa mitungi hiyo ya gesi itasaidia kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusisitiza kuwa kupika kwa gesi ni nafuu ukilinganisha na kuni au mkaa ambao mbele ya safari una madhara Mengi ya kiafya ambayo yatahitaji fedha nyingi kuyatibu.

“Dar es salaam ndio Mkoa unaotumia nishati chafu kutokana na wingi wa watu wanaotumia kuni na mkaa kwa ajili ya kupika hivyo uamuzi huu wa Puma Energy Tanzania unakwenda kumaliza au kupunguza matumizi ya nishati chafu katika Mkoa wetu na Tanzania kwa ujumla.

Akigusia faida za kutumia nishati safi amesema ni pamoja na Kusaidia kuokoa muda mwingi unaotumika kupika kwa kuni na mkaa, kuokoa gharama na kubwa zaidi ni kuepuka madhara ya kiafya yanayosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Puma Energy Tanzania, Fatma Abdallah amesema kampuni hiyo imedhamiria kumuunga mkono Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia na ndio wameitoa mitungi hiyo ambayo itagawanywa katika wilaya zote tanı za Mkoa huo.

“Katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna shughuli  nyingi  miongoni mwa shughuli hizo ni biashara ya chakula kinachoandaliwa kwa wingi kutoka kwa Mama Lishe ambao  wanakumbana na changamoto nyingi, mojawapo ikiwa upatikanaji wa nishati ya kupikia, hususan nishati safi na salama,” ameeleza. 

Amesema Puma Energy Tanzania inaelewa  serikali chini ya Rais Samia imekuwa na mpango kazi kwa miaka kadhaa  wa kuelimisha na kueneza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi wote.

Amesema Jitihada hizo zimejionyesha katika mikutano ya ndani na nje ya nchi ambayo Rais Samia amekuwa akishiriki kuhakikisha upatikanaji na matumizi ya nishatisafi unaimarika.

“Tunatambua wajibu wake wa kushiriki katika masuala ya maendeleo ya jamii, hivyo itaendelea kushirikiana na serikali inayoongozwa na Rais Samia kuhakikisha kampeni ya nishati safi inafanikiwa kwani dhamira ya Rais ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi na sisi tuko naye kufikia malengo hayo,” amesema.


Share on Google Plus

About emmanuel mbatilo

Mahmoud Zubeiry Works at BIN ZUBEIRY "BIN ZUBEIRY" Tangaza nasi hapa.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment