Meneja Bidhaa na Huduma za Kibenki kutoka Benki ya NBC, Jonathan Bitababaje (wa tatu kulia) akiwa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es salaam alioporejea nchini sambamba na baadhi ya wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali nchini waliopata fursa ya kwenda nchini China ili kushiriki Maonyesho ya Uagizaji na Uuzaji wa bidhaa za China maarufu kama Canton Trade Fair kwa uratibu wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kupitia klabu yake ya Biashara ijulikanayo kama NBC B-Club. Wafanyabiashara hao waliwasili jijini Dar es Salaam leo alfajiri baada ya kukamilisha safari hiyo ya siku 10.
Meneja Bidhaa na Huduma za Kibenki kutoka Benki ya NBC, Jonathan Bitababaje (wa pili kulia) akiwatakia heri mara baada ya kurejea nchini baadhi ya wafanyabiashara waliopata fursa ya kwenda nchini China ili kushiriki Maonyesho ya Uagizaji na Uuzaji wa bidhaa za China maarufu kama Canton Trade Fair kwa uratibu wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kupitia klabu yake ya Biashara ijulikanayo kama NBC B-Club. Wafanyabiashara hao waliwasili jijini Dar es Salaam leo alfajiri baada ya kukamilisha safari hiyo ya siku 10.
Sambamba na Maonesho hayo ya Canton Trade Fair yaliyofanyika hivi karibuni Guangzhou, China, wafanyabiashara hao pia walipata fursa ya kukutana na wasafirishaji wa mizigo kutoka China, wazalishaji halisi wa bidhaa mbalimbali ili kujifunza teknolojia mpya sambamba na kutafuta muunganiko mpya wa kibishara na masoko baina yao na wafanyabiashara kutoka China
Aidha, wakiwa njiani kuelekea na kurudi katika safari hiyo wafanyabiashara hao pia walipata wasaa wa kutembelea nchi ya Misri na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii na historia ya taifa hilo.
*******************************
Dar es Salaam: Oktoba 23, 2023: Baadhi ya wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali nchini waliopata fursa ya kwenda nchini China ili kushiriki Maonyesho ya Uagizaji na Uuzaji wa bidhaa za China maarufu kama Canton Trade Fair kwa uratibu wa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kupitia klabu yake ya Biashara ijulikanayo kama NBC B-Club wamerejea nchini huku wakielezea mafanikio, matumaini na fursa mbalimbali walizozipa kupitia safari hiyo.
Sambamba na Maonesho hayo ya Canton Trade Fair yaliyofanyika hivi karibuni Guangzhou, China, wafanyabiashara hao pia walipata fursa ya kukutana na wazalishaji halisi wa bidhaa mbalimbali ili kujifunza teknolojia mpya sambamba na kutafuta muunganiko mpya wa kibishara na masoko baina yao na wafanyabiashara kutoka China.
Aidha, wakiwa njiani kuelekea na kurudi katika safari hiyo wafanyabiashara hao pia walipata wasaa wa kutembelea nchi ya Misri na kujionea vivutio mbalimbali vya utalii na historia ya taifa hilo.
Akizungumza mara tu baada ya kuwasili Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es salaam mapema hii leo, Meneja Bidhaa na Huduma za Kibenki kutoka Benki ya NBC, Jonathan Bitababaje alisema kupitia safari hiyo ya siku 10 wafanyabiashara hao walipata fursa ya kujifunza mambo mengi ikiwemo fursa za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kibiashara huku pia wakipata fursa ya kutembelea viwanda na masoko mbalimbali nchini.
“Zaidi, tukiwa China, tulipata fursa ya kukutana na wafanyabiashara wakubwa, wamiliki wa viwanda vikubwa na vidogo. Pia wafanyabiashara waliweza kujifunza teknolojia mpya sambamba na kupata muunganiko mpya wa kibiashara na wenzao kutoka China. Kuna ambao walihitaji mashine na zana mbalimbali kwa ajili ya kazi zao wamepata na pia wapo waliopata washirika wapya kibiashara. Ni matumaini yetu kwamba hivi karibuni tutashuhudia uwekezaji wao mpya kupitia viwanda,’’ alibainisha.
Kwa mujibu wa Bitababaje wakiwa Guangzhou, China walipata fursa ya kukutana na Konseli Mkuu wa Ubalozi Mdogo wa Tanzania jijini Guangzhou, China Khatib Makenga ambae pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa hatua hiyo muhimu aliwasisitiza Watanzania kutumia vema ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili kwa kuwa na maono ya kuanzisha viwanda nchini Tanzania badala ya kutegemea tu kuagiza bidhaa kutoka China.
“Kwa mujibu wa Mheshimiwa Makenga ni kwamba China kuna teknolojia za ukubwa tofauti hivyo Watanzania wana fursa ya kuangalia teknolojia wanazozimudu ikiwemo teknolojia rahisi itakayowawezesha kuzalisha baadhi ya bidhaa ndogo ndogo hapa hapa nchini ili kupunguza idadi ya bidhaa zinazoingizwa kutoka China.’’ Alinukuu Bitababaje huku akibainisha kuwa benki hiyo ipo tayari kuwasaidia wafanyabiashara hao kwa kuwapatia mitaji itakayowasaidia kuyatimiza kwa vitendo yale yote waliyojifunza nchini China.
‘’Niwaombe sana wafanyabiashara waendelee kuchangamkia fursa ya safari hizi ambazo zinaendelea kuja kupitia uratibu wa NBC B-Club ambapo tunatarajia kuwa na safari nyingine za China mwezi Aprili na Oktoba hapo mwakani. Tofauti na China pia tutakuwa na safari za Ulaya, Asia na baadhi ya nchi za Afrika ambazo tunaushirikiano mkubwa wa kibiashara,’’ aliongeza.
Wakizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara wengine waliopata fursa hiyo Mhandisi Renatusi Porini na Bi Sarah Munuo pamoja na kuishukuru benki ya NBC kwa uratibu wa safari hiyo, walisema wamejifunza mambo mengi ikiwemo pia fursa mpya nyingi za kimasoko na mahusiano ya biashara hatua ambayo imewajenga zaidi kibiashara.
“Kimsigi tulivyorudi leo sio kama tulivyoenda! Tukiwa China na Misri tumetembelea vmaeneo mbalimbali vikiwemo viwanda na pia tumeongeza mawasiliano zaidi na wenzetu wa huko China. Binafsi nikiwa kama mhandisi nimepata ‘materials’ mpya na teknolojia mpya ya ujenzi hatua ambayo ni muhimu sana kwa biashara yangu. Tunawashukuru sana NBC kwa hili hasa tukizingatia kwamba pamoja na hatua hii wametuthibitishia dhamira yao ya dhati kabisa ya kutupatia mikopo ili kukamilisha kwa vitendo haya tuliyojifunza huku,’’ alishukuru Mhandisi Porini.
0 comments:
Post a Comment