MO DEWJI NDIYE BILIONEA KIJANA ZAIDI AFRIKA

Na Nuzulack Dausen, Dar es Salaam
Mfanyabiashara maarufu nchini na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohammed Dewji (pichani) kwa mara ya kwanza ameingia kwenye orodha ya mabilionea 29, akiwa tajiri kijana kuliko wote barani Afrika.
Jarida la Forbes la Marekani limemtaja Dewji (39), katika nafasi ya 24 ya matajiri wa Afrika akiwa na utajiri wa Dola 1.3 bilioni za Marekani (Sh2.34 trilioni) unaotokana na biashara mbalimbali anazozifanya kupitia kampuni yake ya Mohammed Enterprises (Metl Group).
“Dewji alibadilisha biashara aliyoanzisha baba yake kutoka uuzaji bidhaa na kuwa na  viwanda vya Metl,” inasema sehemu ya habari inayomuhusu bilionea huyo Mtanzania iliyochapishwa juzi jioni.

“Alinunua viwanda vya nguo na mafuta vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kwa bei ndogo na kuvifanya viwe na faida zaidi kwa kutumia mtindo wa kisasa wa menejimenti,” inaongeza ripoti hiyo.
Metl ina viwanda vya kutengeneza nguo na bidhaa nyingine za matumizi ya binadamu vikiwamo vyakula, sabuni na vinywaji. Pia ina mapato yanayozidi Dola 1.4 milioni za Marekani (Sh2.5 trilioni) kwa mwaka.
Katika kampuni hiyo, ambayo imekuwa na ushindani dhidi ya kampuni kubwa nyingine kama Said Salim Bakhresa, Dewji anamiliki asilimia 75 ya hisa zote.
Kwa mujibu wa tovuti yake, Metl inaendesha shughuli za uagizaji na usafirishaji bidhaa kutoka na kwenda nje, uzalishaji unaohusisha nguo, vinywaji na vyakula, usagaji nafaka, nishati na  petroli na utengenezaji baiskeli.
Pia inahusika na huduma za simu, fedha, kilimo na pia ina kitengo cha kontena kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Dewji anashika nafasi mbili juu zaidi ya kada maarufu wa CCM na aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Igunga, Aziz Rostam (50) aliyewekwa nafasi ya mwisho. 
Rostam amefungana nafasi ya 26 na mabilionea wa Nigeria, Abdulsamad Rabiu na Femi Otedola wenye utajiri wa Sh1.8 trilioni kila mmoja.
Orodha hiyo ya 29 bora inaoongozwa na bilionea wa Nigeria, Aliko Dangote akiwa na utajiri wa Dola 15.7 bilioni za Marekani (Sh28.2 trilioni), kiwango ambacho ni mara moja na nusu ya bajeti ya Serikali ya Tanzania ya mwaka 2014/15.
Forbes linamtaja Rostam kuwa na utajiri wenye thamani ya Dola 1  bilioni za Marekani (Sh1.8 trilioni), kiwango ambacho kimebaki pasi na mabadiliko kutoka orodha ya mwaka jana.  Rostam anamiliki asilimia 35 ya hisa katika kampuni ya huduma za simu za mkononi ya Vodacom.
Share on Google Plus

About Mahmoud Bin Zubeiry

Mahmoud Zubeiry Works at BIN ZUBEIRY "BIN ZUBEIRY" Tangaza nasi hapa.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment