POLISI YAMSAFISHA ALIYEKAMATWA NA MILIONI 700 DODOMA

Na Dany Tibason, DODOMA
JESHI la polisi mkoa wa Dodoma limetoa taarifa kwamba raia mwenye asili ya kiasia,Amit Kevalramani,aliyekamatwa na fedha zaidi ya Milioni 700 zilikuwa ni fedha zake mwenyewe. 
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, David Misime amesema baada ya uchunguzi uliofanywa na jeshi la polisi walibaini kuwa fedha hizo zilikuwa zake.
“Napenda kutoa taarifa fupi kuhusu tukio lililotokea tarehe 11/07/2015 majira ya saa10:00 asubuhi katika Hoteli ya St. Gasper hapa mjini Dodoma, kuwa wananchi walitoa taarifa majira ya saa 10:00 kwamba kuna mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia amekamatwa na wananchi akiwa na fedha nyingi na kuna vurugu kubwa.

Mabegi mawili yaliyowekwa fedha zilizokamatwa Dodoma

“Baada ya kupata taarifa hizo Jeshi la Polisi Mkoani hapa lilifika eneo la tukio ili kuona kama taarifa hizo ni za kweli.
“Askali walithibitisha kuwa ni kweli walimkuta mtu mmoja mwenye asili ya Kiasia ambaye alijulikana kwa jina la Amit Kevalramani mwenye umri wa miaka 31, Mhindi, Mfanyabiashara, Mkazi wa Dar es Salaam   akiwa na fedha kiasi cha Tsh. 722,500,000.
“Alipohojiwa alisema kuwa tarehe 10/07/2015 alifika Dodoma kwa ajili ya ununuzi wa mazao ya nafaka”alieleza kamanda Misime.
Misime amesema  mtuhumiwa huyo alifika Dodoma 10 Julai mawaka huu majira ya asubuhi na alifikia katika Hoteli ya St. Gasper na 11 Julai 2015 aliamua kurudisha fedha benki kutokana na kuona mkusanyiko wa watu wengi wasioeleweka na wenye viashiria vya vurugu.
Amesema  akiwa katika harakati ya kurejesha fedha hizo benki, ndipo kundi la watu waliokuwa katika eneo la Hoteli ya St. Gasper walimtilia mashaka na kumzuia asiondoke na ndipo taarifa zilitolewa polisi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Misime amesema  mashaka  ya watu hao yalitokana na vuguvugu za kisiasa/mchakato wa uchaguzi kati ya makundi mbalimbali kuwa kuna watu wanahonga wajumbe.
Amesema  taarifa hizo ndizo hata polisi walizopokea kabla ya kufanya uchunguzi lakini baada ya uchunguzi wa kina jeshi hilo lilijiridhisha kuwa taarifa hizo hazikuwa za kweli.
“ Katika tukio hili na uchunguzi tulioufanya tumebaini kuwa hakuna kosa la jinai lililothibitika licha ya kukutwa na kiasi hicho cha fedha, tuhuma za rushwa ambazo ndiyo zilikuwa msingi wa ukamataji wa mtu huyo hazikuthibitika, kwa kuwa hakuna aliyeona akizigawa fedha hizo wala hakuna aliyedai kushawishiwa au kugawiwa fedha hizo.
“Aidha imethibitika fedha hizo ni mali yake halali na kwa kuwa hakuna ushahidi mwingine uliyo thibitisha vinginevyo amerejeshewa fedha zake” alisema Misime
Wakati huo huo Misime amesema 10 Julai 2015 majira ya saa saa 3 usiku eneo la Railway Dodoma tulifanikiwa kuwakamata raia wa Burundi kwa kosa la kuishi nchini bila kibali.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Hererimana Methode(21), Hatungimana Alexis, (20),Niyongabo Justin,( 20),Nteturuye Onesphore (21), Bikorimana Levis, (21) ambao wote ni Wakazi wa Mabanda Burundi kwa kosa la kuingia nchini na kuishi nchini bila kibali.
Amesema  watuhumiwa hao a walikuwa wanasafiri na treni kuelekea Dar es Salaam na walipofika Dodoma Askari wanaosindikiza treni waliwashtukia na walipowakamata na kuwahoji walijieleza kuwa ni raia wa Burundi.
Kutokana na tukio hilo Misime amesema  anawaomba wananchi wa mkoa wa Dodoma na nje ya Dodoma kutoa ushirikiano pale wanapoona watu ambao siyo raia.
Amesema  wasikubali kuwakaribisha wasiwakaribishe bali watoe taarifa kwa vyombo vya dola waweze kuhojiwa kwani hata kama waliingia Nchini na kuhifadhiwa katika makambi yaliyopo Nchini hawaruhusiwikutoka kwenda mbali na  kambi  zao bila kuwa na kibali maalum. 
Share on Google Plus

About Mahmoud Bin Zubeiry

Mahmoud Zubeiry Works at BIN ZUBEIRY "BIN ZUBEIRY" Tangaza nasi hapa.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment